TANZANIA, JAPAN KUENDELEA KUSHIRIKIANA KUPUNGUZA VIFO VINAVYOTOKANA NA AJALI ZA BARABARANI
Posted on: July 10th, 2026Na Zakayo Mosha – WAF, Dodoma
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Japan ili kuboresha huduma za dharura pamoja na kuendeleza elimu ya usalama barabarani kwa wananchi kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi elimu ya juu, ikiwa ni mkakati wa kupunguza vifo na madhara yatokanayo na ajali za barabarani nchini.
Hayo yamesemwa leo, Julai 10, 2026, jijini Dodoma na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Eliud Eliakimu, wakati wa kikao cha wataalamu wa Wizara ya Afya, Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA) pamoja na Wizara ya Ujenzi.
Akizungumza katika kikao hicho, Meneja wa Mradi, Bw. Manabu Ohno, amesema mradi huo umeanza Aprili 2025 na unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu hadi mwaka 2028 na kuelezea kuwa mradi unalenga kutoa elimu kuhusu matumizi salama ya barabara kwa wananchi, hususan wanafunzi kuanzia shule za awali na msingi.
Dkt. Eliakimu amesema mafanikio ya mradi huo yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya wizara na taasisi mbalimbali ili kuhakikisha unawafikia Watanzania wengi zaidi na kuchangia kufikiwa kwa malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kupunguza vifo na madhara yatokanayo na ajali za barabarani ifikapo mwaka 2030.
"Ili mradi huu uendelee kufanikiwa na kuwafikia Watanzania wengi zaidi, juhudi na ushirikiano wa pamoja kati ya wizara za kisekta unahitajika ili kuhakikisha malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kupunguza vifo na madhara yatokanayo na ajali za barabarani yanafikiwa ifikapo mwaka 2030," alisema Dkt. Eliakimu.
Aidha, amewataka wataalamu kuendelea kukamilisha mikakati ya kitaalamu kwa kushirikiana na wizara na taasisi zinazohusika na huduma za dharura zitokanazo na ajali za barabarani, ili kuhakikisha kunakuwa na mwelekeo mmoja katika utoaji wa huduma na mawasiliano kwa umma.
"Wizara ya Afya tutaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi salama ya barabara kwa kushirikiana na wizara nyingine, pamoja na kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ili kufikisha ujumbe kwa wananchi wote wa Tanzania," amesisitiza.