SERIKALI YAIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA UKIMWI, KIFUA KIKUU KUPITIA UWEKEZAJI WA SEKTA YA AFYA
Posted on: July 31st, 2026Na Andrea Kadege, WAF-Dodoma
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughukikia Dawa na Vifaa Tiba, Bw. Emmanuel Tayari amesema Serikali imeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya Kifua Kikuu na UKIMWI kupitia uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya ikiwemo kuboresha hali ya upatikanaji wa dawa uimarishaji wa uwezo wa ndani wa uzalishaji wa dawa, hatua ambazo zimechangia kupungua kwa maambukizi na vifo vinavyotokana na magonjwa hayo nchini.
Bw. Tayari ameyasema hayo leo Julai 31, 2026 Jijini Dodoma wakati akifunga kikao cha kutathmini uboreshaji wa huduma za UKIMWI, Kifua Kikuu na Huduma Muunganisho za afya ,kikao ambacho kimewajumuisha Waganga Wakuu wa Mikoa, Waratibu wa Huduma za Maabara, Wafamasia na Waratibu wa Huduma za UKIMWI.
Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma za afya kupitia miradi ya kimkakati inayolenga maisha ya mwananchi, akisisitiza kuwa "Taifa linaloagiza dawa zote kutoka nje halijiamulii afya yake lenyewe, linaazima"
"Serikali imetenga shilingi bilioni 180 kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi pamoja na shilingi bilioni 250 kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya, huku ikiendelea kuwekeza katika uzalishaji wa dawa ndani ya nchi, ikiwemo kiwanda cha dawa za kufubaza Virusi Vya UKIMWI" amesema Bw. Tayari
Katika hatua nyingine amebainisha kuwa kiwango cha maambukizi ya VVU kimeendelea kupungua, idadi ya watu wanaopata dawa za kufubaza virusi imeongezeka, na vifo vinavyotokana na UKIMWI vimepungua, maambukizi mapya ya kifua kikuu yameendelea kushuka huku kiwango cha mafanikio ya matibabu kikiongezeka, akisisitiza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa Serikali, wataalamu wa afya na wadau mbalimbali wa sekta ya afya.
Aidha, ameongeza kuwa kutokana na uwekezaji huo, viongozi katika ngazi hizo wanayo nafasi nzuri zaidi ya kuleta mabadiliko kutokana na uwepo wa dawa, vifaa tiba, mifumo ya kidijitali, takwimu sahihi na Serikali yenye dhamira ya kuendelea kuimarisha huduma za afya.