UNYONYESHAJI MAZIWA YA MAMA NCHINI WAONGEZEKA NA KUFIKIA ASILIMIA 64
Posted on: August 1st, 2026Na Aisha Swahibu, WAF - Tanga
kiwango cha unyonyeshaji maziwa ya mama nchini Kimezidi kuimarika,ambapo watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee wameongezeka kutoka asilimia 58 mwaka 2018 hadi asilimia 64 mwaka 2022.
Hayo yameelezwa leo Agosti 1, 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mhe. Dadi Kolimba akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian,wakati akifungua maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa mtoto duniani yaliyoanza leo Agosti 1 na kutarajiwa kutamatika Agosti 8, 2026, jijini Tanga
Mhe. Dadi amesema watoto wanaoanza kunyonya ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa wameongezeka kutoka asilimia 53.5 mwaka 2018 hadi asilimia 70 mwaka 2022, jambo linaloonesha mafanikio ya juhudi za kuhamasisha unyonyeshaji nchini.
Mhe. Dadi amesisitiza umuhimu wa kumsaidia mama kuendelea kunyonyesha hadi angalau mtoto afikishe miaka miwili huku akibainisha bado kuna changamoto ya kuendelea kunyonyesha baada ya mtoto kufikisha mwaka mmoja,
“Serikali inaendelea kutekeleza sera, sheria na kanuni zinazolinda haki za uzazi, ikiwemo likizo ya uzazi, muda wa kunyonyesha kazini na ulinzi dhidi ya ubaguzi ili kuwawezesha wanawake kunyonyesha kwa usalama.
Aidha, Mhe. Dadi amewataka Viongozi, waajiri, taasisi, wadau wa maendeleo na jamii kwa ujumla kushirikiana katika kuweka mazingira rafiki yanayowawezesha wanawake kunyonyesha na kutekeleza haki zao za uzazi.
Katika hatua nyingine, amewahimiza wanaume kushiriki kikamilifu katika kumsaidia mama kwa kumpatia msaada wa kihisia, kijamii na kiuchumi ili kufanikisha unyonyeshaji na kuboresha afya ya mama na mtoto.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe Wizara ya Afya Bi. Neema Joshua ameeleza kuwa mtoto anapozaliwa chakula sahihi cha kumpatia ni maziwa ya mama miezi sita ya mwanzo baada ya hapo aanzishiwe vyakula vya nyongeza hii itamsaidia mtoto kuwa na Afya bora na ukuwaji mzuri
“ Ajenda ya lishe ni kipaumbele kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani ni matamanio yake ya kuwa na taifa lenye Afya bora,” amesema Bi. Neema