MRADI WA KUPAMBANA NA ATHARI ZA JOTO KWENYE MICHUANO YA AFCON KUCHOCHEA UCHUMI WA NCHI
Posted on: August 5th, 2026Na Emmanuel Maleg, WAF – DSM
Uwepo wa mradi wa kupambana na athari za joto kwenye michuano ya AFCON nchini umetajwa kuchochea uchumi wa nchi kwa kuwawezesha wanamichezo, wafanyakazi na washiriki watakaohudhuria mashindano hayo kukabiliana na joto kwa kupata bidhaa mbalimbali.
Hayo yamesemwa leo Agosti 5, 2026 jijini Dar Es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa huduma za kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Otilia Gowelle wakati akifungua semina elekezi kwa wataalam kutoka sekta mbalimbali wanaohusika moja kwa moja katika maandalizi ya kukabiliana na athari za joto.
Dkt. Gowelle amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) zinasaidiana kuandaa nyenzo za utayari ili kuhakikisha mashindano ya AFCON 2027 yanaweza kufanyika kulingana na mapendekezo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).
“Kupatikana kwa mradi wa “Beat the Heat” katika maandalizi ya mashindano ya AFCON umekua kama ni chachu ya kuinua uchumi wa nchi kwani utasaidia kutoa elimu kwa washiriki namna ya kujikinga na athari za joto na kujengewa uelewa wa mavazi ya aina gani wanatakiwa kuvaa au kutumia vinywaji gani na kwa wakati gani wakiangalia mpira”, amesema Dkt. Gowelle.
Dkt. Gowelle ameongeza kuwa kumekua na baadhi ya mashabiki kuanguka uwanjani baada ya timu zao kupata matokeo fulani, Hali hiyo husababishwa na wananchi kutokua na utayari wa kushiriki katika matukio ya michezo kwa kutojiandaa kunywa au kula au kusongamana katika maeneo yenye watu wengi.
Aidha, ili kuepuka athari hizo amewataka washiriki katika semina hiyo kujifunza namna ya kuwasiliana na washiriki wa michezo ikiwemo mashabiki kuwapa elimu ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza viwanjani.
Naye, Dkt. Neema Kileo ambaye alimuwakilisha Mwakilishi Mkazi wa WHO nchini amesema Shirika la Afya Duniani liliingia makubaliano na FIFA katika mashindano mbalimbali ambapo nchi muandaaji inatakiwa kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kulinda afya za washiriki kupitia mradi wa kulinda afya kwenye sekta ya michezo ya “Beat the Heat”.