WIZARA YA AFYA KUWAFIKIA MAELFU YA VIJANA KUPITIA MABONANZA YA AFYA YA UZAZI
Posted on: August 3rd, 2026Na Abdu Madenge, WAF – MOROGORO
Wizara ya Afya imeanza kikao kazi cha kupitia na kuboresha jumbe za afya ya uzazi zitakazotumika kuwafikia maelfu ya vijana katika mabonanza makubwa yatakayofanyika mkoani Mwanza na Ruvuma mwezi Agosti mwaka huu.
Kikao hicho kinachofanyika kuanzia Agosti 3 hadi 7, 2026 mkoani Morogoro, kimeratibiwa na Idara ya Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kupitia Programu ya Afya ya Uzazi kwa Vijana, kikihusisha wataalamu wa afya pamoja na wadau wanaotekeleza Afua za afya ya Uzazi kwa Vijana.
Lengo la kikao hicho ni kuhakikisha jumbe zitakazotolewa wakati wa bonanza zinakuwa sahihi, zenye kuzingatia ushahidi wa kitaalamu na zinazoendana na mahitaji ya vijana wa sasa ili kuongeza uelewa kuhusu afya ya uzazi, kuhimiza matumizi ya vituo vya huduma rafiki kwa vijana na kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi yanayolinda afya na mustakabali wao.
Mabonanza hayo yanatarajiwa kufanyika katika jamii na Vyuo mbalimbali kuanzia Agosti 23, 2026 mkoani Ruvuma na Mwanza ambapo yatajumuisha michezo tofauti,huku yakijumuisha utoaji wa elimu ya afya ya uzazi kwa Vijana, huduma za ushauri na upimaji wa afya kwa lengo la kuwafikia vijana wengi zaidi katika mazingira rafiki.
Serikali kupitia Wizara ya Afya imelenga kutumia mabonanza haya kama jukwaa la utoaji elimu na sehemu ya mkakati wa kuimarisha mawasiliano ya mabadiliko ya tabia kwa kuwafikia vijana wengi zaidi kupitia mbinu zinazowavutia na kuwawezesha kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo katika kipindi cha ujana balehe na Ujana,baadhi ya changamoto ni mimba katika umri mdogo, lishe duni, uelewa hafifu wa njia za kupanga Uzazi, maambukizi ya VVU, magonjwa ya ngono na homa ya Ini, Ukatili wa kijinsia na changamoto ya Afya ya akili.
Kupitia kikao hicho, washiriki wanapitia na kuboresha jumbe mbalimbali zitakazotumika wakati wa mabonanza ili kuhakikisha zinatoa elimu yenye tija, zinazohamasisha tabia chanya na kuongeza mwitikio wa vijana kutumia huduma za afya ya uzazi zinazotolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.