Wizara Ya Afya

TEKNOLOJIA IHUSISHWE KUKUZA ELIMU YA LISHE NA UNYONYESHAJI

Posted on: August 3rd, 2026

Na Aisha Swahibu, WAF – Tanga

Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe Bi. Neema Joshua ameeleza matumizi sahihi ya teknolojia yana nafasi kubwa katika kuboresha huduma za afya, hususan kwenye masuala ya lishe na unyonyeshaji wa maziwa ya mama, huku akitoa wito kwa wananchi kuitumia kupata na kusambaza taarifa sahihi zinazolinda afya za jamii.

Bi. Neema amesema hayo leo Agosti 3, 2026 mkoani Tanga wakati akifungua kikao kazi cha kuhamasisha na kuimarisha mkakati wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama .

Amesema teknolojia imekuwa nyenzo muhimu katika ukusanyaji na ufuatiliaji wa takwimu za lishe, unyonyeshaji na huduma nyingine za afya, hivyo kuchangia kupanga na kuboresha huduma kwa wananchi huku akutaja changamoto ya matumizi mabaya ya teknolojia kupitia usambazaji wa taarifa zisizo sahihi zinazoweza kupotosha jamii kuhusu afya, na kusisitiza kuwa kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha anatumia majukwaa ya kidijitali kwa uwajibikaji.

“Tunakubali na kuthamini matumizi ya teknolojia kwa sababu ni sehemu ya maendeleo ya dunia ya sasa. Kinachohitajika ni kuhakikisha inatumika kwa usahihi ili wananchi wapate taarifa sahihi zinazowasaidia kufanya maamuzi bora kuhusu afya zao,” amesema Bi. Neema.

Aidha, Bi. Neema ameeleza kuwa unyonyeshaji wa maziwa ya mama ni mojawapo ya njia muhimu za kupunguza vifo vya watoto wachanga na wale walio chini ya miaka mitano, sambamba na kupunguza tatizo la utapiamlo ambalo linaweza kuanza mtoto akiwa bado tumboni endapo mama hatapati lishe na huduma stahiki.

Amesisitiza kuwa mtoto anapaswa kupata matunzo bora tangu anapozaliwa, ikiwemo kunyonyeshwa maziwa ya mama ipasavyo, ili kuhakikisha anakua akiwa na afya njema kimwili na kiakili.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha afua za lishe na unyonyeshaji ili kujenga taifa lenye watoto wenye afya bora, uwezo wa kujifunza, kufikiri na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.

Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani yanaanza Agosti 1 hadi 7kila mwaka, Tanzania imekuwa ikiadhimisha wiki hiyo tangu mwaka 2002 kwa lengo la kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa afya, ukuaji na maendeleo