MAWASILIANO JUMUISHI MSINGI WA KUTOKOMEZA MALARIA NCHINI
Posted on: July 27th, 2026Na Atley Kuni, WAF – Morogoro
Mawasiliano jumuishi yametajwa kuwa nguzo muhimu ya kufanikisha juhudi za Serikali za kutokomeza malaria nchini ifikapo mwaka 2030 kwa kutoa taarifa sahihi kwa wananchi wakiwemo watu wenye ulemavu wa kuona na uziwi kwa wakati na kwa njia zinazokidhi mahitaji yao.
Mkuu wa Mawasiliano sehemu ya Malaria Wizara ya Afya Bi. Leah Ndekuka, amesema hayo leo Julai 27, 2026 wakati akitoa maelezo ya utangulizi kwenye kikao kazi cha siku tano kilichoandaliwa na Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP) kwa ajili ya kupitia na kuandaa jumbe, vielelezo vya uhamasishaji wa malaria vinavyolenga watu wenye ulemavu wa kuona na kusikia.
"Nyenzo zitakazoandaliwa zinapaswa kuwa rahisi kueleweka na kuzingatia mahitaji ya walengwa ili kuongeza uelewa kuhusu mbinu za kujikinga na malaria pamoja na matumizi sahihi ya afua mbalimbali zinazotolewa na Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo," amesema Bi. Ndekuka
Aidha, Bi. Ndekuka amesema kuwa ushirikishwaji wa wadau mbalimbali wakati wa kuandaa jumbe na vielelezo hivyo utasaidia kuzalisha maudhui yenye ubora, yanayokubalika na yanayowafikia walengwa kwa ufanisi, huku akisisitiza kuwa uzoefu na maoni ya washiriki ni sehemu muhimu ya mafanikio ya mchakato huo.
Katika kikao hicho, washiriki wanapitia jumbe zilizopo, kutoa mapendekezo ya maboresho na kujadili mbinu bora za kuwasilisha taarifa za malaria kwa watu wenye ulemavu wa kuona na usikivu kwa lengo la kuhakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma katika utoaji wa elimu ya afya.
Bi. Ndekuka amewaasa washiriki kutumia utaalamu wao na kushiriki kikamilifu katika mijadala ili kuhakikisha kikao kinazalisha nyenzo bora zitakazotumika katika kampeni mbalimbali za uhamasishaji wa malaria nchini.
Kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali wanaoshiriki katika kuboresha mawasiliano ya afya na kinatarajiwa kuandaa jumbe na vielelezo vitakavyoongeza upatikanaji wa taarifa za malaria kwa watu wenye ulemavu, hatua inayochangia kuimarisha ushiriki wa makundi yote ya jamii katika juhudi za kudhibiti na hatimaye kutokomeza malaria nchini ifikapo mwaka 2030.