SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA UFADHILI WA AFYA, YASISITIZA BIMA YA AFYA KWA WOTE: DKT. MWIGULU
Posted on: September 9th, 2026Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali itaendelea kuimarisha ufadhili wa sekta ya afya na kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya bila kujali hali zao za kipato.
Dkt. Mwigulu amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Huduma za Afya ya Msingi unaofanyika jijini Arusha, leo Septemba 9, 2026 kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ni sehemu muhimu ya jitihada za Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa gharama nafuu, huku akiwataka Watanzania wote wenye uwezo kushiriki katika mfumo huo.
“Bima ya afya ni ya wote. Maana yake ni kila Mtanzania anapaswa kushiriki katika mfumo huu ili kupitia ushiriki huo ndipo tutakapoweza kuwa na bima jumuishi ambayo haitamuacha mtu nyuma,” amesema Dkt. Mwigulu
Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa Bima ya Afya kwa Wote haipaswi kuchukuliwa kama mpango wa misaada unaolenga watu wasiojiweza pekee, bali ni mfumo unaohitaji ushiriki wa wananchi wote na kujenga mfuko imara na endelevu wa kugharamia huduma za afya.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutafuta vyanzo vya mapato ili kuongeza wigo wa wananchi watakaonufaika na mpango huo, huku ikiendelea kusaidia kaya ambazo hazina uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali tayari imeweka zaidi ya shilingi bilioni 48 kwa ajili ya utekelezaji wa awali wa Bima ya Afya kwa Wote, mpango ulioanza kutekelezwa Januari 2026.
Dkt. Mwigulu ameitaka jamii kuendelea kujiunga katika Bima ya Afya kwa Wote ili kuhakikisha hakuna Mtanzania anayeachwa nyuma katika upatikanaji wa huduma za afya.