Wizara Ya Afya

SERIKALI, WADAU WAIMARISHA URATIBU WA AFYA MOJA NCHINI

Posted on: September 8th, 2026

Na Cletus Sanga, WAF – Arusha

Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI kwa kushirikiana na CIHEB Tanzania chini ya Mradi wa Usalama wa Afya Duniani imeendelea kuimarisha uratibu wa utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Taifa wa Afya Moja, unaolenga kuimarisha uwezo wa nchi kukabiliana na vihatarishi vya afya.

Akizungumzia umuhimu wa mpango huo leo Septemba 8,2026, mkoani Arusha, Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Afya Moja kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Salum Manyatta, amesema dhana ya Afya Moja inahitaji ushirikiano wa sekta na taaluma ili kuzuia na kukabiliana na milipuko ya magonjwa.

“Lengo la dhana ya Afya Moja ni kupanua na kuimarisha ushirikiano baina ya sekta na taaluma mbalimbali kwenye hatua zote za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na milipuko ya magonjwa na hatari nyingine za afya zinazohitaji ushiriki wa sekta zaidi ya moja na taaluma mbalimbali,” amesema Dkt. Manyatta.

Amesema, Mpango Mkakati wa Taifa wa Afya Moja umeainisha maeneo sita ya msingi ya utekelezaji ambayo ni uratibu kujiandaa na kukabiliana na majanga; ufuatiliaji, utambuzi na uzuiaji, utafiti, elimu na mafunzo,pamoja na uhamasishaji, utetezi na mawasiliano.

Amesema Kamati za Kiufundi zimeundwa ili kuwawezesha wataalamu kutoka sekta mbalimbali kujadili na kuratibu utekelezaji wa majukumu katika maeneo hayo.

Dkt. Manyatta ameongeza kuwa, dhana hiyo inaunganisha afya ya binadamu, wanyama na mazingira, huku ikisisitiza matumizi ya pamoja ya taarifa na rasilimali katika kukabiliana na milipuko ya magonjwa, usugu wa vimelea dhidi ya dawa na changamoto nyingine za afya ya jamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mradi wa Usalama wa Afya Duniani (Global Health Security – GHS) kutoka CIHEB Tanzania, Dkt. Edgar Lusaya, amesema CIHEB Tanzania itaendelea kushirikiana na Serikali kupitia kujenga uwezo wa wataalamu, kuimarisha mifumo ya uratibu na kusaidia utekelezaji wa mikakati ya kukabiliana na vihatarishi vya afya