Wizara Ya Afya

DKT. SAMIZI AKABIDHI VIFAA VYA USAIDIZI WA USIKIVU KWA WATOTO 15

Posted on: September 9th, 2026

Na Shaban Juma, WAF – Arusha

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amekabidhi vifaa vya usaidizi wa usikivu kwa watoto 15 waliobainika kuwa na changamoto ya usikivu wakati wa Kambi ya Madaktari Bingwa iliyofanyika mwezi Julai mwaka huu.

Dkt. Samizi amekabidhi vifaa hivyo leo Septemba 09, 2026 jijini Arusha, ambapo vifaa hivyo vimegharamiwa na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, kwa gharama ya zaidi ya Shilingi milioni 37, kwa lengo la kuwasaidia watoto hao kuboresha uwezo wao wa kusikia na hatimaye kuboresha maisha yao.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha watoto wanaobainika kuwa na changamoto za kiafya wakati wa kambi za madaktari bingwa wanaendelea kupata huduma zinazohitajika hadi pale wanapopata suluhisho la changamoto zao.

Aidha, Dkt. Samizi akiwa katika Hospitali hiyo amekagua utolewaji wa huduma za afya pamoja na hali ya utayari wa hospitali katika kukabiliana na mahitaji ya huduma, hususan katika kipindi ambacho Mkoa wa Arusha unatarajiwa kupokea wageni wengi mwaka 2027 watakaokuja nchini kushiriki mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Amesema maandalizi hayo ni muhimu ili kuhakikisha mkoa huo unakuwa tayari kutoa huduma bora, salama na kwa wakati kwa wananchi pamoja na wageni watakaofika nchini wakati wa mashindano hayo.

Dkt. Samizi amewataka watendaji wa sekta ya afya mkoani Arusha kuendelea kuboresha utoaji wa huduma na kuimarisha maandalizi katika maeneo yote muhimu, ikiwemo upatikanaji wa vifaa tiba, dawa, wataalamu na miundombinu ya afya.

Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Afya, itaendelea kuimarisha huduma za afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na zinazokidhi mahitaji yao.