Wizara Ya Afya

UWEKEZAJI HUDUMA ZA AFYA YA MSINGI WASISITIZWA, KUFIKIA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Posted on: September 9th, 2026

Na Aisha Swahibu, WAF-Arusha

Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki Kati na Kusini imesema uwekezaji huduma za afya ya msingi ni nguzo muhimu katika kufikia azma ya kuwa na huduma bora, jumuishi na zinazopatikana kwa usawa kwa wananchi wote, huku nchi za Afrika zikihimizwa kuimarisha mifumo ya afya, nguvu kazi, teknolojia na rasilimali fedha kwa ajili ya kuendeleza huduma hizo.

Hayo yamesemwa Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki Kati na Kusini Dkt. Ntuli Kapologwe, wakati wa kutoa salam kwenye Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Huduma za Afya ya Msingi unaofanyika Arusha, leo Septemba 9, 2026,

Dkt. Ntuli amesema Tanzania ina historia ya kipekee ya utekelezaji wa huduma za afya ya msingi, ambapo juhudi hizo zilianza mwaka 1967 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Azimio la Arusha, kabla ya Azimio la Alma-Ata la mwaka 1978 na kuipa dunia dira ya Afya kwa Wote kwa kuweka huduma za afya ya kuwa msingi wa upatikanaji wa huduma za afya kwa usawa na kwa wote.

“Changamoto zinazoikabili dunia kwa sasa zinahitaji nchi kutafakari upya namna ya kuimarisha huduma za afya ya msingi, ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo wa ndani wa taasisi, rasilimali watu, mifumo ya ufadhili na matumizi ya teknolojia,” amesema Dkt. Ntuli

Amesisitiza kuwa dhana ya uhuru wa kiafya haimaanishi kujitenga, bali kujenga uwezo wa nchi na mifumo yake ya afya kukabiliana na changamoto na kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki.

Aidha, Dkt. Ntuli amesisitiza kuwa umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa na kikanda ili kuimarisha huduma za afya ya msingi, akitaja ushirikiano na Shirika la Afya Duniani (WHO), pamoja na mashirika ya kikanda na jumuiya za afya barani Afrika. Amesema ushirikiano huo unatoa fursa kwa nchi kujifunza na kubadilishana uzoefu na kuimarisha mifumo ya afya, ikiwemo Tanzania, Kenya na Rwanda.

Dkt. Ntuli ametoa wito kwa wadau wote kuongeza uwekezaji wa huduma za afya ya msingi, akieleza kuwa uwekezaji huo ni muhimu kwenye kufikia huduma ya afya kwa wote, kuimarisha usalama wa mifumo ya afya duniani na kuendeleza ajenda ya afya kupitia diplomasia na ushirikiano wa kimataifa.