Wizara Ya Afya

WATAALAMU WA MAABARA WAENDELEA KUIMARISHWA KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MLIPUKO

Posted on: September 7th, 2026

Na Zakayo Mosha – WAF, Morogoro

Wataalamu wa maabara kutoka vituo vya afya vya Serikali na binafsi kwa mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Pwani, Lindi, Mtwara na Morogoro wameanza mafunzo ya siku tano, kuanzia Septemba 7 hadi 11, 2026, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, ikiwemo Ebola.

Kauli hiyo imetolewa leo, Septemba 7, 2026, mjini Morogoro na Salum Nyanga, mtaalamu kutoka Maabara ya Taifa na ambaye pia ni Meneja Msaidizi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, wakati akieleza maandalizi yaliyofanyika kuelekea ufunguzi rasmi wa mafunzo hayo unaotarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 8, 2026.

Amesema wataalamu hao wa maabara wana jukumu la kusimamia na kutoa taarifa za magonjwa yanayofuatiliwa kutoka ngazi ya msingi hadi mikoa husika.

Kwa mujibu wa Nyanga, kupitia mafunzo hayo watajengewa uwezo kuhusu namna bora ya ukusanyaji, uchakataji na usafirishaji salama wa sampuli za magonjwa ya mlipuko, kwa lengo la kuimarisha usalama wa watumishi wa afya na wananchi.

Aidha, amesema kuwa mafunzo hayo yanatarajiwa kufunguliwa rasmi siku ya Jumanne, Septemba 8, 2026, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Msajili kutoka Bodi ya Maabara Binafsi za Afya.

Amesisitiza kuwa hatua hiyo inaonesha jinsi Serikali, kupitia Wizara ya Afya, inavyothamini mchango wa sekta binafsi katika kuboresha huduma za afya nchini.

Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma za Maabara, Sehemu ya Uchunguzi, Ufuatiliaji na Udhibiti wa Magonjwa (Laboratory-Based Surveillance) kutoka Wizara ya Afya, Bw. Joakim John Chacha, amesema mafunzo hayo ni mwendelezo wa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya na wadau wa maendeleo, hususan Shirika la Afya Duniani (WHO), kupitia mradi wa *Pandemic Fund*.

“Ni matarajio yangu kuwa baada ya mafunzo haya ya siku tano kukamilika, siku ya Ijumaa, Septemba 11, 2026, wataalamu watakuwa na ujuzi, maarifa pamoja na weledi zaidi katika ukusanyaji, utunzaji, uchakataji na usafirishaji wa sampuli kwa njia bora na salama, ili kulinda afya za watumishi wa afya na wananchi,” amesema Bw. Chacha.