Wizara Ya Afya

TANZANIA YAHIMIZA UFADHILI WA NDANI KUFIKIA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Posted on: September 8th, 2026

Na Andrea Kadege, WAF - Arusha

Tanzania imehimiza kuimarisha ufadhili wa ndani wa sekta ya afya ili kupunguza utegemezi wa misaada ya nje na kuhakikisha huduma bora na endelevu za afya kwa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa katika Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Huduma za Afya ya Msingi (IPHCC2026), na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Dkt. Zeyana Hamid, leo Septemba 9, 2026, jijini Arusha, akitaja mkutano huo kama fursa ya kujadili changamoto na mikakati ya kufikia Afya kwa Wote.

Amesema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unahitaji kuongeza mapato ya ndani na matumizi bora ya rasilimali, huku afya ikiangaliwa kwa mtazamo wa kisekta unaohusisha pia usalama wa chakula, ustawi wa jamii na maendeleo ya kiuchumi.

Dkt. Zeyana amesema, Tanzania, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeanza utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wot, huku na akisisitiza umuhimu wa kuwekeza kwenye uzalishaji wa ndani wa dawa na vifaa tiba ili kupunguza gharama, kuongeza ajira na kuimarisha uwezo wa nchi.

Amesema Afrika inapaswa kubadilika kutoka kuwa muagizaji wa bidhaa za afya na kuwa mzalishaji na msambazaji ndani ya bara, na kupendekeza kuangaliwa vyanzo vya ziada vya mapato kupitia kodi za kiafya, ikiwemo kwenye tumbaku, pombe na vinywaji vyenye sukari.

Mkutano huo pia unalenga kuimarisha ushirikiano wa nchi na wadau mbalimbali katika kuboresha huduma za afya ya msingi, ikiwemo kuongeza uwekezaji, kuimarisha mifumo ya afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya zilizo bora, salama na zinazopatikana kwa usawa bila kujali hali zao za kiuchumi au maeneo wanayoishi.