Wizara Ya Afya

MWONGOZO WA MATIBABU YA MAGONJWA YA MILIPUKO YANAYOSABABISHA KUTOKWA NA DAMU WAHUISHWA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: July 31st, 2026

Na Happyness Hans, WAF - Morogoro

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura, Dkt. Michael Kiremeji amesema kikao kilichoanza Julai 27 na kuhitimishwa leo Julai 31, 2026, mkoani Morogoro, kimefikia hatua nzuri katika kuhuisha mwongozo wa matibabu ya magonjwa ya milipuko yanayosababisha kutokwa na damu.

Akizungumza leo Julai 31, 2026, mkoani Morogoro, Dkt. Kiremeji amesema lengo la kikao hicho ni kuwa na mwongozo mmoja wa pamoja utakaotumika katika kukabiliana na magonjwa yote ya milipuko yanayosababisha kutokwa na damu.

Amebainisha kuwa uhuishaji wa mwongozo huo umezikutanisha taasisi mbalimbali, hospitali na wadau wa maendeleo wakiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO), CDC na AMREF. Aidha, mwongozo huo pia utawasaidia wataalamu wa afya kujiandaa kutoa huduma stahiki endapo magonjwa hayo, ikiwemo Ebola na Marburg, yatatokea nchini.

Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Janeth Masuma amesema uwepo wao mkoani Morogoro ni sehemu ya ushirikiano na Wizara ya Afya katika kuboresha mwongozo wa matibabu ya wagonjwa wa magonjwa ya milipuko yanayosababisha kutokwa na damu, ikiwemo Marburg na Ebola.

Amesema WHO imeendelea kushirikiana na Wizara ya Afya kuhakikisha huduma za afya zinazotolewa kwa wananchi zinakuwa bora zaidi, hususan katika kipindi hiki ambacho baadhi ya nchi jirani zinakabiliwa na milipuko ya magonjwa hayo.

Naye Daktari Bingwa na bingwa Bobezi wa Magonjwa ya Ndani pamoja na Magonjwa ya Moyo (Cardiology) kutoka Hospitali ya KCMC, Dkt. Gisela Nyakunga amesema huu ni wakati sahihi wa kuhuisha mwongozo huo kwa kuwa utakuwa na manufaa makubwa kwa nchi na utawasaidia watumishi wa afya kukabiliana na magonjwa hayo endapo yataingia nchini.