Wizara Ya Afya

USIMAMIZI SHIRIKISHI WAIMARISHA UBORA WA HUDUMA ZA AFYA HOSPITALI YA RUFAA YA MOUNT MERU

Posted on: July 27th, 2026

Na Cletus Sanga, WAF – Arusha

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na CIHEB Tanzania kupitia Mradi wa Usalama wa Afya Duniani (Global Health Security Project) imefanya usimamizi shirikishi katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru mkoani Arusha kwa lengo la kuimarisha ubora wa huduma za afya, kuongeza utayari wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko pamoja na kuimarisha utekelezaji wa viwango vya kinga na udhibiti wa maambukizi.

Hayo yamebainishwa leo, tarehe 27 Julai 2026, na Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru, Dkt. Mlambo Kipapi, wakati wa kupokea timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya na CIHEB Tanzania iliyofanya usimamizi shirikishi katika hospitali hiyo. Mkoani Arusha

Amesema zoezi hilo limeiwezesha hospitali kutathmini utendaji wake, kubaini maeneo yanayohitaji maboresho na kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya zilizo salama, zenye ubora na zinazokidhi viwango vya kitaifa.

Dkt. Kipapi ameongeza kuwa wataalamu wamepitia utekelezaji wa miongozo mbalimbali ya huduma za afya, mifumo ya kinga na udhibiti wa maambukizi, utayari wa kukabiliana na dharura za afya ya umma pamoja na utoaji wa ushauri wa kitaalamu kwa watumishi wa afya ili kuendelea kuboresha utendaji katika hospitali hiyo na kuimarisha usalama wa wagonjwa.

Kwa upande wake, Afisa Muuguzi kutoka Wizara ya Afya ambaye pia ni Mratibu wa zoezi hilo, Bi. Theresia Haule, amesema usimamizi shirikishi ni nyenzo muhimu inayowezesha wataalamu kutathmini utekelezaji wa miongozo ya kitaifa, kubaini changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzitatua ili kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Bi. Haule ameongeza kuwa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na CIHEB Tanzania itaendelea kufanya usimamizi shirikishi katika hospitali na vituo vingine vya kutolea huduma za afya nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo wa watumishi, kuimarisha kinga na udhibiti wa maambukizi, kuongeza utayari wa kukabiliana na dharura za afya ya umma na kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma bora, salama na zenye viwango vinavyokubalika.