Wizara Ya Afya

MAFUNZO KWA WATAALAMU WA AFYA YAONGEZA UTAYARI WA KUKABILIANA NA EBOLA- MAWENZI

Posted on: July 28th, 2026

Na Mwandishi wetu, WAF – Kilimanjaro

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri mkuu TAMISEMI na CIHEB Tanzania chini ya Mradi wa Usalama wa Afya Duniani, imeendelea kuimarisha uwezo wa watumishi wa afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi, mkoani Kilimanjaro, kupitia mafunzo yanayolenga kuboresha mifumo ya utoaji wa huduma za afya, kuongeza uzingatiaji wa miongozo ya kitaifa na kuimarisha utayari wa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola.

Akizungumza tarehe 28 Julai, 2026, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Jairy Khanga amesema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha watumishi wa afya wanatoa huduma bora kwa kuzingatia mifumo na miongozo ya kitaifa ya utoaji wa huduma.

Amesema mafunzo hayo yataongeza ufanisi wa utendaji kazi, kuboresha uratibu wa huduma, kuimarisha usalama wa wagonjwa na wahudumu wa afya pamoja na kuhakikisha hospitali inakuwa na utayari wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Dkt. Khanga amesema washiriki wamepatiwa ujuzi kuhusu matumizi sahihi ya vifaa kinga binafsi (PPE), kanuni za kuzuia na kudhibiti maambukizi (IPC), utambuzi wa dalili za awali za ugonjwa wa Ebola, usimamizi wa wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na maambukizi pamoja na hatua za kuchukua ili kuzuia kusambaa kwa maambukizi ndani ya vituo vya kutolea huduma za afya.

Kwa upande wake, Mratibu wa Usimamizi wa Wagonjwa, Bi. Laura Marandu, amesema mafunzo hayo yameongeza uelewa wa watumishi wa Afya kuhusu usimamizi wa wagonjwa kwa kuzingatia miongozo ya kitaifa na kimataifa, jambo litakalosaidia kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa kwa wagonjwa na kuongeza usalama wao pamoja na usalama wa wahudumu wa afya.

Bi. Marandu amesema washiriki pia wamejengewa uwezo wa kuzuia na kudhibiti maambukizi, matumizi sahihi ya vifaa kinga binafsi, kuimarisha ushirikiano wa timu za afya na kufuata miongozo ya utoaji wa huduma ili kuhakikisha wagonjwa wanapatiwa huduma salama na zenye ubora hata wakati wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, ikiwemo Ebola.