Wizara Ya Afya

MAFUNZO KWA VITENDO YAIMARISHA UWEZO WA WAHUDUMU WA AFYA KUKABILIANA NA EBOLA - SAME

Posted on: August 3rd, 2026

Na Cletus Sanga, WAF – Kilimanjaro

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na CIHEB Tanzania chini ya Mradi wa Usalama wa Afya Duniani imeendelea kuimarisha uwezo wa watumishi wa afya katika Hospitali ya Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, kupitia mafunzo yanayolenga kuboresha huduma za dharura, kuongeza uzingatiaji wa miongozo ya kitaifa na kuimarisha utayari wa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola.

Akizungumza leo Agosti 04, 2026, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Same, Dkt. Bilisia Brown, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kujenga uwezo wa wataalamu wa afya ili kuhakikisha hospitali zinakuwa tayari kutoa huduma salama na zenye ubora wakati wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa.

Amesema mafunzo hayo yameongeza uwezo wa watumishi kutumia miongozo ya kitaifa katika utoaji wa huduma za dharura na kuimarisha uratibu wa huduma ndani ya hospitali.

Dkt. Brown amesema washiriki wamepatiwa mafunzo ya vitendo kuhusu utambuzi wa mapema wa wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na Ebola, matumizi sahihi ya vifaa kinga binafsi , utekelezaji wa kanuni za kuzuia na kudhibiti maambukizi, usimamizi wa wagonjwa mahututi pamoja na mbinu za kuzuia maambukizi kusambaa ndani ya vituo vya kutolea huduma za afya.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Michael Kiremeji, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Wizara za kuendelea kuimarisha utayari wa vituo vya kutolea huduma za afya nchini katika kukabiliana na dharura za afya ya umma, ikiwemo milipuko ya magonjwa.

Amesema kuwajengea uwezo wataalamu wa afya kunahakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa hata wakati wa majanga ya kiafya.