SIKU YA SIKOSELI DUNIANI, TAKWIMU BADO ZIKO JUU NCHINI
Posted on: June 19th, 2025
Na WAF, Dar es Salaam
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoshika takwimu za juu duniani ikishika nafasi ya nne kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa selimundu ikitanguliwa na Nigera, India na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kuwa zaidi ya watoto 300,000 huzaliwa na Sikoseli kila mwaka duniani huku Tanzania peke yake watoto takribani 14,000 huzaliwa na ugonjwa huo kwa mwaka sawa na watoto 14 kati ya kila watoto 1,000.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Toba Nguvila akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalage amesema ugonjwa huo unasababishwa na kurithi vinasaba vyenye hilafu kutoka kwa wazazi wote wawili.
Kiongozi huyo wa mkoa wa Dar es Salaam pia amebainisha kuwa takwimu zinaonesha kuwa karibu watoto saba (7) kati ya 100 wenye umri chini ya miaka mitano hufariki kutokana na madhara ya ugonjwa huo.
Aidha Dkt. Nguvila ameongeza kuwa juhudi za Serikali kupambana na ugonjwa huo ni pamoja na upatikanaji wa vipimo vya haraka, dawa za hydroxyurea, Pen V na folic acid akivitaja hupatikana katika ngazi ya hospitali za wilaya.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Wizara ya Afya Dkt. Ahmad Makuwani amesema ugonjwa huo unasababisha maumivu makali ikiwemo homa, uharibifu wa viungo na wakati mwingine vifo usipodhibitiwa mapema au kugunduliwa mapema.
Dkt. Makuwani ameongeza kuwa kwa sasa kama nchi tunabahati kwani kupitia juhudi za pamoja kati ya Serikali, wahudumu wa afya, na wadau mbalimbali wameshuhudia maendeleo makubwa katika utambuzi, matibabu, na uhamasishaji wa jamii.
"Vituo vya huduma nchini vimeendelea kuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma bora kwa wagonjwa wa selimundu ikiwa ni pamoja na huduma za kliniki maalum,ushauri nasaha, na usambazaji wa dawa zinazosaidia kudhibiti dalili za ugonjwa huu," ameongeza Dkt Makuwani.
Kauli mbiu ya Maadhimisho haya ni Hatua madhubutiza Kitaifa kwa matokeo chanya ya kijamii kuwezesha jamii kujitambua kuzuia na kukabiliana na sikoseli hivyo kusadifu kusudio la Serikali la kuhamasisha na kujenga uelewa kuhusu ugonjwa huo.