SERIKALI, WADAU KUENDELEA KUELIMISHA VIJANA NA JAMII NCHINI MASUALA YA AFYA YA UZAZI
Posted on: August 6th, 2026Na Zakayo Mosha WAF -Morogoro
Wizara ya Afya kupitia Idara ya huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto programu ya afya ya uzazi kwa vijana kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi imeendelea kutoa elimu kwa vijana na jamii ya Watanzania kwa ujumla kuhusiana na masuala ya afya ya uzazi kwa lengo la kujenga jamii yenye afya bora ya uzalishaji katika kukuza Maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya familia na Taifa.
Hayo yamesemwa leo Agosti 6, 2026 mjini Morogoro na Afisa programu Mama na Mtoto wa Wizara ya Afya Bi. Notgera Ngaponda wakati akifunga kikao kazi cha siku nne kilichokutanisha Wataalam wa afya na wadau mbalimbali kupitia jumbe za afya kwa vijana zitakazotumika kuelimisha vijana katika mabonanza yatakayofanyika hivi karibuni katika Mkoa wa Ruvuma na Mwanza.
Amewashukuru washiriki hao kwa kufanya kazi nzuri katika muda wote wa kikao na hivyo kuwezesha maandalizi mengine kuendelea, amesema wazazi, walezi na jamii kwa ujumla bado wanajukumu kubwa la kuwaelimisha vijana kuelewa vema kuhusu masuala ya afya kwa ujumla ili waweze kukabili changamoto za afya wanazokutana nazo.
"Napenda kuwashukuru wadau mbalimbali wanaoendelea kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya kuhakikisha kuwa, vijana wetu wa kitanzania wanapata elimu iliyos ahihi tena Kwa wakati ya afya kwa vijana, naomba wadau wengi zaidi kuendelea kujitokeza ili kufanikisha mpango huu muhimu wa kujenga jamii imara na Taifa lenye ustawi mzuri wa afya," amesema na kuongeza Bi.Notgera.
Kwa upande wake Bw. Denice Simeo mratibu wa afua za vijana na ujumuishi wa makundi Maalum kutoka Shirika linalojishughulisha na afya ya uzazi Tanzania (MSI-Tanzania) amesema kuwa, vijana wakitanzania bado wanahitaji elimu zaidi ya masuala ya uzazi,hivyo amewataka wadau wengine kuunga mkono juhudi za Serikali kupitia Wizara ya afya za kuwaelimisha masuala ya uzazi na kuwafikia vijana wengi zaidi waishio mijini na vijijini.
"Kama Shirika la MSI Tanzania tumeamua kwa dhati kushirikiana na Wizara ya Afya kutoaji elimu ya Afya ya uzazi kwa vijana baada ya kuona na kugundua kuwa, vijana wanakabiliana na changamoto nyingi ikiwemo mimba katika umri mdogo, Magonjwa ya ngono na ukimwi pamoja na changamoto ya ukuaji na makuzi kwani kundi la vijana linaathirika sana" amesema Bw.Denice.
Aidha, ametoa wito kwa wadau wengine wanaojishughulisha na masuala ya Afya ya uzazi kuongeza juhudi zaidi za utoaji elimu ili kunusuru kundi hili kubwa la vijana kwa lengo la kujenga Taifa imara lenye vijana ambao watakuja kujenga leo yao na Kesho yao kwa manufaa yao ,familia zao na Taifa kwa ujumla wake.
Kukamilika kwa kikao kazi hiki ni hatua muhimu ya mafanikio inayoendelea kuchukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya , Idara ya huduma za afya ya uzazi ,Mama na Mtoto katika programu ya afya ya uzazi kwa vijana kwa lengo la kufanikisha tukio muhimu la utoaji wa elimu kwa Vijana kupitia mabonanza katika Mikoa ya Ruvuma na Mwanza.