SERIKALI YAENDELEA KUHAKIKISHA UWEPO WA VYANZO VYA UHAKIKA, UTEKELEZAJI WA BIMA YA AFYA KWA WOTE
Posted on: August 12th, 2026Na Hassan Kimweri, WAF – Dodoma
Serikali inaendelea kuhakikisha uwepo wa vyanzo vya uhakika vya kugharamia huduma za afya ili kuwezesha utekelezaji endelevu wa Bima ya Afya kwa Wote na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya bila ya kuwa na kikwazo cha fedha.
Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Florence Samizi amesema hayo leo Agosti 12, 2026 wakati akijibu maswali ya Wabunge wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Dkt. Johannes Lukumay, baada ya kuwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.
"Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imejikita katika kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya njema na wanapata huduma za matibabu, huku Serikali ikiweka utaratibu wa kuwahudumia wananchi wasio na uwezo wa kugharamia bima," amesema Dkt. Samizi
Aidha, Dkt. Samizi amesema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote umeanza kwa awamu ili kuiwezesha Serikali kuimarisha mifumo muhimu ikiwemo utambuzi wa kaya, upatikanaji wa dawa, mifumo ya malipo na utoaji wa huduma, kabla ya kwenda katika utekelezaji mpana zaidi.
“Maana yake ni kwamba mwenye uwezo atalipa, asiye na uwezo atalipiwa na Serikali, tunacholenga ni kuhakikisha wananchi wote wanakuwa na bima na wanapata huduma wanapozihitaji bila kuwa na kikwazo cha fedha,” amesema Dkt. Samizi
Pia, Naibu Waziri Dkt. Samizi amesema utekelezaji wa awamu ya mwanzo umeisaidia Serikali kupata uzoefu na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho, ikiwemo kuimarisha mifumo katika ngazi ya msingi ya huduma za afya ambako wananchi wengi hupata huduma.
Amesema, ni muhimu wananchi kuelewa kuwa bima ya afya ni kinga dhidi ya gharama kubwa za matibabu na kwamba elimu inapaswa kutolewa kwa wananchi ili wawe na bima kabla ya kuugua, badala ya kusubiri wanapopata matatizo ya kiafya.
Mwisho, Dkt. Samizi ametoa wito kwa Wabunge na wadau mbalimbali kushirikiana na Serikali kutoa elimu kuhusu umuhimu wa bima ya afya, akisisitiza kuwa mfumo wa kuchangia unasaidia kuhakikisha wananchi wanaougua wanapata matibabu bila kubeba gharam