TANZANIA, AFRICA50 WAINGIA MAKUBALIANO YA KUBORESHA SEKTA YA AFYA
Posted on: August 6th, 2026Na Hassan Kimweri, WAF – Dar es Salaam
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya imeingia makubaliano ya ushirikiano na Shirika la Africa50 Project Finance yenye lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini kwa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Makubaliano hayo yamesainiwa mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Agosti 6, 2026 kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe na Bw. Djalal Khimdjee kwa niaba ya Africa50 Project Finance katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, wakati wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika.
Makubaliano hayo yamelenga maeneo makubwa manne ambayo ni kuongeza matibabu ya magonjwa ya figo ikiwemo uchujaji damu na upandikizajaji, kuboresha huduma za kinga, tiba na tiba shufaa ya magonjwa ya Saratani, kuwezesha sekta binafsi kuongeza uzalishaji wa bidhaa za afya na dawa ndani ya nchi pamoja na kuboresha huduma za upasuaji wa ubongo, mishipa ya fahamu, mgongo na huduma za urekebishaji (Rehabilitation).
Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha ushirikiano na taasisi za kimataifa katika kuwekeza kwenye miundombinu ya afya na kuboresha huduma za ubingwa, ubingwa bobezi na utoshelevu wa bidhaa za afya nchini.
Makubaliano hayo yanaendeleza juhudi za Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuvutia ushirikiano wa kimataifa na uwekezaji unaochochea maendeleo ya sekta ya afya na kuboresha ustawi wa wananchi.