Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI KUIWEZESHA MIREMBE KUIMARISHA HUDUMA ZA MSINGI ZA AFYA YA AKILI

Posted on: June 6th, 2024
  1. Na WAF - DODOMA


Wizara ya Afya kuiwezesha Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe kuimarisha huduma za msingi za afya ya akili kupatikana maeneo mbalimbali nchini ili kuboresha hali ya utoaji wa huduma. 


Hayo yamebainika Juni 5, 2024 Jijini Dodoma wakati wa  zoezi la usimamizi shirikishi wa hospitali ya Taifa ya afya ya akili Mirembe zoezi lililoongozwa na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya Dkt. Hamad Nyembea 


Dkt. Nyembea  amesema hospitali hiyo ina jukumu kubwa nchini la kuimarisha huduma za msingi za afya ya akili kupatikana maeneo mbalimbali nchini, kwa kuwafikia waanzishaji wa huduma za msingi katika ngazi ya mkoa.


”Hapa mnatoa huduma za kibingwa lakini kuna huduma zingine nyingi zinakuja apa ambazo sio hadhi yenu, sasa inabidi tusaidie kwenda kutibu kule ili wagonjwa wengi wapate huduma mapema tena kulekule, tunaweza tukaanza kwa kushirikiana na nyie, kwanza tuanze na mpango wa muda mfupi miaka mitatu walau baada ya muda fulani baadhi ya hizi huduma zipatikane maeneo mengi” amesema Dkt. Nyembea 


Amesema Serikali itawasaidia ili waweze kufikisha huduma hizo katika ngazi ya msingi kwa kuzingatia pia vipaumbele vya hospitali hiyo vya uimarishaji kinga ya magonjwa ya afya ya akili kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kuzuia magonjwa ya akili, Kuimarisha tafiti na matumizi ya matokeo ya tafiti mbalimbali za Afya katika kufanya maamuzi, Kuimarisha uwezo wa taasisi wa kutoa huduma; na Kuimarisha utoaji wa huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi.


“Sasa hili ni jukumu letu sote, kama wanataaluma tutawategemea muweze kulifikisha hili kwa kwa ngazi ya msingi ili na zile Huduma za Msingi ziweze kupatikana kirahisi na kwa wahitaji wote, sababu sasa hivi kama nchi tuna pambana kufikia kila kona” ameongeza Dkt. Nyembea


Awali wakati akisoma taarifa ya hospitali hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe Dkt. Paul Lawala ameishukuru serikali kwa kuiwezesha hospitali hiyo Kuwapeleka masomoni wataalam waliopo ili waweze kuongeza ujuzi na ufanisi na kuwa mabingwa na mabingwa bobezi wa magonjwa ya akili lakini pia ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya iongeze ruzuku ya dawa kwa Hospitali ili kuweza kumudu gharama zinazohitajika kwa wagonjwa wasioweza kumudu kuchangia huduma.


“Hospitali inawasiliana na wadau ili kushirikiana nao au kupata fedha za kuendeshea programu za kuielimisha jamii kuhusu afya ya akili, Kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa ushiriki wao katika mchakato wa matibabu na mtengamao kwa wagonjwa wa afya ya akili, Kugharamia ukarabati mdogo wa miundombinu, vifaa na vifaa tiba ili kuwezesha utolewaji wa huduma. Kufanya ukarabati wa majengo ya kutolea huduma, kujenga baadhi ya majengo na njia za kuunganisha majengo (walk ways) katika mwaka huu wa fedha (2023/2024) na Kutoa elimu kwa wateja kuhusu upatikanaji wa huduma za Afya ya Akili katika ngazi za msingi ya huduma za afya” amesema  Dkt Lawala.


Mwisho.