Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATAALAM WA MAABARA WATAKIWA KUHAKIKISHA UBORA WA SAMPULI UNAENDANA NA UWEKEZAJI UNAOFANYWA NA SERIKALI

Posted on: June 25th, 2025

Na WAF - MOROGORO.


Serikali imeagiza wataalam wa Maabara nchini kuhakikisha menejimenti na uandaaji wa Sampuli unazingatia ubora na kuendana na  uwekezaji ambao unafanywa Serikali ili kuongeza ufanisi kwa maabara ya taifa.


Wito huo umetolewa na Mganga Mkuu wa  Mkoa wa Morogoro, Dkt. Best Magoma leo Juni 25 2025 mkoani Morogoro   wakati akifungua mafunzo ya menejimenti ya sampuli na upimaji wa magonjwa ya mlipuko nchini kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe.


Amesema Serikali imefanya mabadiliko makubwa katika maeneo ya kutolea huduma za maabara kwa kuwekeza vifaa na rasilimali mbalimbali, kwa kuboresha miundombinu pia wataalam wamendelea kuzalishwa na kujengewa uwezo kwa  kupewa ufadhili tofauti na hali ilivyokuwa awali huku lengo kuu likiwa ni kuboresha hali ya ubora wa huduma za maabara nchini.



“Baada ya mafunzo haya tupate ushuhuda kutoka kwa wenzetu wa Maabara ya taifa  kwamba sampuli zinazokuja kutoka maabara za mikoa zimezidi kuwa bora na kuimarika, kulingana na uwekezaji na rasilimali ambazo Serikali inatumia katika kuboresha huduma za Maabara nchini,” amesema Dkt. Magoma.


Naye Mkuu wa huduma za Maabara kutoka Wizara ya Afya Bw. Reuben Mkala amesema ni imani yake baada ya mafunzo hayo maabara nchini zitakuwa na uwezo wa kuboresha huduma hususani mikoa 10 ambayo imeanza kupokea mafunzo hayo na pia kuwezesha wenzao kwa kuanzia hospitali za Rufaa za mikoa mpaka ngazi ya Afya msingi.



Kwa upande wake Mratibu wa Huduma za ufuatiliaji Magonjwa na Dharura Maabara, Bw. Joakim Chacha amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais - TAMISEMI zinaendelea kutekeleza juhudi za kuboresha huduma za maabara kwa kuwajengea uwezo wataalam wake kitaaluma, ili kuongeza ufanisi na kufikia viwango vya ubora vinavyotakiwa hasa wakati wa dharura za milipuko ya magonjwa.


“Kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Mpox kwa baadhi ya mikoa, yameandaliwa  mafunzo haya maalum kwa wataalam wa maabara kutoka mikoa nane (8) ambayo ni Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Lindi, Mbeya, Tanga, Geita, na Simiyu, ili kuwaimarisha katika ukusanyaji, uandaaji, uhifadhi, usafirishaji na upimaji wa sampuli kwa kuzingatia miongozo ya kitaifa na kimataifa,” amesema Bw. Chacha.