WANANCHI SHINYANGA WAOMBA KUONGEZEWA SIKU ZA MADAKTARI BINGWA WA SAMIA
Posted on: June 25th, 2025
Na WAF, Shinyanga
Wananchi mkoani Shinyanga wameomba kama kuna uwezekano wa kuongezwa siku za Madaktari Bingwa na Bobezi wa Rais Samia ili changamoto za Afya zinazowakabili ziweze kutatuliwa.
Hali hiyo imejitokeza Juni 25, 2025 ikiwa ni siku tatu tu, tangu kuanza kwa kambi ya madaktari bingwa wa Rais Samia mkoani hapo.
"Hatujui kwa wingi wetu huu kama kweli hizi siku sita zilizopangwa kama zitatutosha kama unavyoweza kuona Umati huu wa watu waliokuja kupata huduma za kibingwa," amesema Mzee John Mandu mkazi wa Chamaguha mkoani Shinyanga.
Kwa uoande wake Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo ya Manispaa Dkt. Moshi Ryioba amesema kumekuwa na ongezeko la idadi ya watu ikilinganishwa na siku zingine ambazo hazikuwa na Madaktari Bingwa.
"Tumepokea wananchi waliokuja kwa siku moja 167, hii sio hali ya kawaida kwani idadi ya kawaida huwa ni watu kati ya 50 hadi 70 kwa siku za kawaida," amesema Dkt. Ryioba.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji Dkt. Boazi Mwasambili kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, amekiri kupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wenyeji wake na kufanikisha Operesheni mbili huku akijiandaa kufanya zingine nne (4).
"Kama unavyoweza kuona hapa nipo na wataalam wawili, ambao tumekuwa nao bega kwa bega tangu siku ya kwanza kuna siku tulitoka hapa karibu saa mbili za usiku lakini hawajaacha kunipatia ushirikiano wakutosha," amesema Dkt. Mwasambili.
Madaktari Bingwa walioweka kambi katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga ni pamoja na Daktari bingwa Watoto, Wanawake, Upasuaji, Pua, Koo na Sikio, Magonjwa ya ndani, Meno pamoja na Wauguzi Mabingwa.