Wizara Ya Afya

TANZANIA KUENDELEZA MAGEUZI YA KIDIGITALI, KUWEKEZA KATIKA RASILIMALI WATU KATIKA SEKTA YA AFYA

Posted on: July 16th, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF - Dar es Salaam

Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi nyingine za Afrika pamoja na wadau katika kuimarisha uongozi, kuwekeza katika rasilimali watu katika sekta ya afya, kuendeleza mageuzi ya kidijitali, kuimarisha utungaji wa sera na kukuza ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za elimu na asasi za kiraia ili kujenga mifumo imara na endelevu ya afya barani Afrika.

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi amesema hayo leo Julai 15, 2026 kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa, wakati akitoa salamu za Serikali katika Mkutano wa Nne wa 'Mkapa Legacy Summit' uliofanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 20 ya Benjamin William Mkapa Foundation.

"Serikali inatambua mchango mkubwa wa Benjamin William Mkapa Foundation katika kuimarisha sekta ya afya nchini kwa kipindi cha miaka 20 kupitia uwekezaji katika rasilimali watu, kuboresha huduma za afya, kuimarisha taasisi pamoja na kushiriki katika maendeleo ya sera mbalimbali za afya," amesema Mhe. Samizi

Aidha, Dkt. Samizi amesema Serikali chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wadau wa maendeleo imechangia uwezeshaji wa zaidi ya watumishi wa afya 19,000 wakiwemo wahudumu wa Afya agazi ya jamii zaidi ya 11,000, kuimarisha Programu ya Mkapa Fellows na kutoa ufadhili wa masomo kwa wataalamu wa afya.

"Sekta ya afya kwa sasa ina takribani watumishi wa afya 182,430, hatua iliyopunguza kwa kiasi kikubwa upungufu wa watumishi na kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya nchini, hususan katika maeneo yaliyokuwa na changamoto ya upungufu wa wataalamu," amesema Dkt. Samizi

Pia, Dkt. Samizi amesema kuwa Serikali imeendelea kuboresha hospitali, vituo vya afya na zahanati, kuongeza vifaa tiba vya kisasa pamoja na kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali ya taarifa za afya, ambayo imeongeza ufanisi katika upangaji, uwajibikaji na utoaji wa maamuzi yanayotegemea ushahidi.