TUENDELEE KUWEKEZA KWA VIJANA NA KUIMARISHA MIFUMO YA AFYA AFRIKA
Posted on: July 16th, 2026Na Hassan Kimweri, WAF – Dar es Salaam
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema Afrika inapaswa kuendelea kuwekeza kwa vijana na kuimarisha mifumo ya afya ili kujenga jamii yenye afya bora na kuhakikisha maendeleo endelevu yanayowanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
Dkt. Nchimbi amesema hayo leo Julai 16, 2026 wakati akifunga rasmi mkutano wa 'Mkapa Legacy Summit 2026' uliofanyika kwa siku Tatu katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalim Julias Kambarage Nyerere jijini Dar es Salaam.
"Benjamin William Mkapa Foundation imeendelea kuwa mshirika muhimu wa Serikali katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za afya kwa kuimarisha huduma za afya, kuendeleza rasilimali watu na kushirikiana na wadau mbalimbali kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili sekta hii," amesema Dkt. Nchimbi
Akizungumzia kaulimbiu ya mkutano ya “From Legacy to Future: Leadership, Health Systems and Youth-led Human Capital for Africa”, Dkt. Nchimbi amesema kaulimbiu hiyo inatoa mwelekeo sahihi wa namna ambavyo Afrika inapaswa kuandaa viongozi wa kesho kwa kuwekeza katika elimu, afya na maendeleo ya vijana.
Aidha, Dkt. Nchimbi amesema uwekezaji katika rasilimali watu, hususan vijana, ndio msingi wa ubunifu, uzalishaji na ukuaji wa uchumi, akieleza kuwa bara la Afrika lina fursa kubwa kutokana na idadi kubwa ya vijana wake endapo watawezeshwa kupata elimu, ujuzi na mazingira ya kufikia ndoto zao.
"Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya kuimarisha sekta ya afya kupitia uwekezaji katika miundombinu, rasilimali watu, mageuzi ya kisera na kuimarisha ushirikiano na taasisi mbalimbali zinazochochea maendeleo ya sekta hiyo," amesema Dkt. Nchimbi
Pia, Dkt. Nchimbi ametoa wito kwa washirika wa maendeleo, taasisi za umma na binafsi pamoja na wadau wa afya kuendelea kushirikiana katika kuwekeza kwenye mifumo ya afya na kuwawezesha vijana ili Afrika iweze kujitegemea katika kukabiliana na changamoto za afya na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.