WIZARA YA AFYA, UNICEF ZAWEKA AFUA KUIMARISHA KINGA DHIDI YA MAGONJWA
Posted on: July 16th, 2026Na Andrea Kadege, WAF-Dodoma
Wizara ya Afya kupitia Idara ya Kinga imekutana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kujadili na kuweka mikakati ya kuimarisha kinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko kupitia kikao kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Afya zilizopo Mtumba , jijini Dodoma leo Julai 16, 2026.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Msaidizi Afya, mazingira na Usafi, Wizara ya Afya Dkt. Amour Seleman, amesema majadiliano hayo yamelenga kutathmini utekelezaji wa shughuli za ushirikiano baina ya Wizara na UNICEF na kuweka vipaumbele vya utekelezaji kwa mwaka 2026/27 kwa maeneo ya afya ya mazingira, maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi ili kuimarisha kinga na utayari wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
"Pande zote tumekubaliana kuendelea kuimarisha uwezo wa watumishi kupitia mafunzo, kuboresha mifumo ya ufuatiliaji na ukusanyaji wa takwimu, pamoja na kuendeleza mawasiliano ya afya kwa umma na afua za kuzuia na kudhibiti magonjwa ya kuambukiza" amesema Dkt. Amour
Dkt. Amour amesisitiza umuhimu wa kuimarisha matumizi ya maji salama ya kunywa, unawaji mikono kwa maji tiririka na sabuni, pamoja na kuboresha usafi katika kaya, shule na maeneo mengine ya jamii, hatua zitakazochangia kupunguza hatari ya magonjwa kama kipindupindu na kuimarisha utayari wa kukabiliana na vitisho vya magonjwa kama Ebola.
Kwa upande mwingine, wajumbe wa kikao hicho wameadhimia kukamilisha mpango kazi utakaoratibu utekelezaji wa vipaumbele vilivyowekwa, huku Wizara ya Afya na UNICEF zikiendelea kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha shughuli hizo zinatekelezwa kwa ufanisi na zinatoa matokeo yanayolenga kulinda afya za wananchi.
Akihitimisha kikao hicho, Dkt. Amour amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na washirika wa maendeleo una mchango mkubwa katika kuimarisha mifumo ya kinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko, kuboresha afya ya mazingira na kuongeza uwezo wa taifa wa kuzuia, kugundua na kukabiliana na dharura za afya kwa wakati.