Wizara Ya Afya

WANAHABARI KIGOMA KUTUMIA KALAMU ZAO KUIELIMISHA JAMII KUHUSU TAHADHARI DHIDI YA EBOLA

Posted on: July 22nd, 2026

Na Atley Kuni, WAF – Kigoma

Wanahabari mkoani Kigoma wamehimizwa kutumia kalamu zao na majukwaa mbalimbali ya habari kuelimisha jamii kuhusu njia za kujikinga na ugonjwa wa Ebola, ili kuongeza uelewa wa wananchi na kusaidia kuzuia hofu pamoja na kusambaa kwa taarifa potofu.

Wito huo umetolewa leo, Julai 22, 2026, mkoani Kigoma wakati wa mafunzo ya uelimishaji kuhusu utayari na tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko yanayoratibiwa na Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI na mdau CIHEB Tanzania kupitia Mradi wa Usalama wa Afya Duniani.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Muelimishaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Gaidon Haule amesema wanahabari ni wadau muhimu katika kulinda afya ya jamii kwa kuhakikisha taarifa sahihi na zenye kuaminika zinawafikia wananchi kwa wakati.

Amesema kupitia habari, vipindi vya redio na televisheni pamoja na majukwaa ya kidijitali, wanahabari wana nafasi ya kuhamasisha wananchi kutambua dalili za Ebola, kufuata kanuni za kujikinga na kutoa taarifa mapema kwa mamlaka za afya endapo watabaini dalili zinazohisiwa kuwa za ugonjwa huo.

"Tunawaomba wanahabari mtumie taaluma yenu katika kuelimisha jamii kwa kuandika habari zenye usahihi, kupinga upotoshaji wa taarifa na kuhamasisha wananchi kuchukua tahadhari zinazotolewa na wataalamu wa afya," amesema Haule

Kwa upande wake, Mratibu wa dawati la elimu kwa Umma mkoa wa Kigoma Abedi Mtau, amesema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kujenga uelewa wa jamii kuhusu masuala ya afya ya umma, hivyo ushiriki wa wanahabari katika kampeni za elimu utasaidia wananchi kupata taarifa sahihi na kupunguza hofu isiyo na msingi.

Baadhi ya wanahabari walioshiriki mafunzo hayo Ezra Lonka chombo cha Main Fm Kigoma na
Naomi Milton wa Redio Kwizera Fm, wameahidi kutumia kalamu zao kwa weledi kuendelea kuandika na kurusha habari zitakazosaidia jamii kuelewa hatua za kujikinga dhidi ya Ebola na magonjwa mengine ya mlipuko.