Wizara Ya Afya

USHIRIKIANO WA KIKANDA NGUZO MUHIMU KUIMARISHA HUDUMA ZA KIBINGWA NA UBINGWA BOBEZI

Posted on: July 20th, 2026

Na Andrea Kadege, WAF -Arusha

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Bw. Emmanuel Tayari, amesema ushirikiano wa kikanda baina ya Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA Health Community) unaendelea kuwa chachu ya kuimarisha huduma za afya, hususan huduma za kibingwa na ubingwa bobezi zinazolenga kuwafikia wananchi kwa wakati.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa tiba, vifaa vya upasuaji na bidhaa za afya kwa ajili ya Kambi ya Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi ya ECSA Jijini Arusha Julai 20, 2026, Bw. Tayari amesema Serikali imepokea vifaa hivyo ili kuboresha utoaji wa huduma za ubingwa na bobezi katika kambi zilizoratibiwa na ECSA Health Community katika Hospitali ya Mt. Meru Arusha na Hospitali ya Kanda ya Kusini Mtwara.

"Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwekeza katika kuimarisha huduma za kibingwa kupitia ushirikiano na taasisi za kikanda, sekta binafsi na wadau wa maendeleo, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora karibu na maeneo wanayoishi" amesema Bw. Tayari

Ameeleza kuwa vifaa vilivyokabidhiwa vitatumika katika Kambi ya Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi ya ECSA itakayotoa huduma mbalimbali za kibingwa, ikiwemo upasuaji wa kibingwa, uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali, pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya kupitia ubadilishanaji wa uzoefu.

Ameongeza kuwa baada ya makabidhiano hayo, kambi za huduma za kibingwa zitaanza zikilenga kuwafikia wananchi ambao wamekuwa wakisubiri huduma za upasuaji na matibabu ya kibingwa kwa muda mrefu, hivyo kupunguza rufaa zisizo za lazima na gharama za kusafiri kutafuta huduma hizo.

Aidha, amesisitiza kuwa changamoto za mifumo ya afya zinahitaji nguvu za pamoja kupitia ushirikiano wa serikali, sekta binafsi, taasisi za kitaaluma na washirika wa maendeleo, akieleza kuwa ushirikiano huo ni msingi wa kujenga mifumo imara ya afya na kuongeza upatikanaji wa huduma bora.