Wizara Ya Afya

UWEKEZAJI KWA VIJANA, WATAALAMU WA AFYA NI MSINGI WA MUSTAKABALI WA AFRIKA

Posted on: July 16th, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF – Dar es Salaam

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Prof. Mohamed Yakub Janabi, amesema uwekezaji katika vijana na rasilimali watu wa afya ni nguzo muhimu ya kujenga mifumo imara ya afya na kuhakikisha maendeleo endelevu barani Afrika.

Prof. Janabi amesema hayo leo Julai 16, 2026 katika Mkutano wa 'Mkapa Legacy Summit 2026 uliofanyika Dar es Salaam katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalim Julias Kambarage Nyerere na kuhudhuriwa na nchi zaidi ya 25 za Afrika.

"Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa, aliamini kuwa uongozi ni huduma kwa wananchi na si fursa ya kutumikiwa, kwa zaidi ya miaka 20, Benjamin William Mkapa Foundation imeendelea kutafsiri falsafa hiyo kwa vitendo kupitia kuimarisha huduma za afya," amesema Prof. Janabi

Amesema, mafanikio makubwa ya taasisi hiyo hayaonekani tu katika takwimu, bali katika maisha ya watu walioguswa na programu zake, akitolea mfano wauguzi na madaktari wanaochagua kufanya kazi katika maeneo yenye uhitaji mkubwa pamoja na wabunifu wa teknolojia za afya wanaorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza kuhusu nguvu kazi ya afya, Prof. Janabi amesema Dunia inatarajiwa kukabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi wa afya ifikapo mwaka 2030, huku Afrika ikiwa miongoni mwa maeneo yatakayobeba mzigo mkubwa zaidi.

"Hali hii inahitaji uwekezaji wa haraka katika mafunzo, ajira, mazingira bora ya kazi na fursa za maendeleo ya taaluma kwa wataalamu wa afya ili kukabiliana na changamoto hiyo itakapojitokeza," amesema Prof. Janabi

Aidha, Prof. Janabi amesema kuwa pamoja na ongezeko la idadi ya wahitimu wa kada za afya barani Afrika, bado kuna changamoto ya wataalamu wengi kutafuta ajira nje ya bara kutokana na mazingira bora zaidi ya kazi.

"WHO inaendelea kushirikiana na nchi wanachama kutekeleza Ajenda ya Rasilimali Watu wa Afya Afrika ya mwaka 2026–2035 yenye lengo la kuongeza uzalishaji wa wataalamu wa afya, kuwaajiri, kuwahifadhi na kuwawezesha kutoa huduma bora ili kufanikisha huduma za afya kwa wote na kuimarisha usalama wa afya," amesema Prof. Janabi