Wizara Ya Afya

ECSA HC YAWEZESHA MILIONI 265 KUIMARISHA HUDUMA ZA UPASUAJI ARUSHA, MTWARA.

Posted on: July 20th, 2026

Na Andrea Kadege – WAF, Arusha

Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA Health Community) imewezesha shilingi milioni 265 kupitia vifaa tiba, vifaa vya upasuaji na bidhaa za afya kwa ajili ya kufanikisha Kambi ya Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi itakayofanyika kuanzia Julai 20 hadi 30, 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mount Meru, Arusha, na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini, Mtwara.

Kambi hiyo inalenga kusogeza huduma za kibingwa na ubingwa bobezi karibu na wananchi, kupunguza rufaa zisizo za lazima pamoja na kuwapatia wagonjwa huduma za matibabu na upasuaji ndani ya maeneo yao.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo iliyofanyika Jijini Arusha leo Julai 20, 2026 Mkurugenzi Mkuu wa ECSA Health Community, Dkt. Ntuli Kapologwe, amesema kambi hiyo itatoa huduma mbalimbali za kibingwa na ubingwa bobezi, ikiwemo huduma za upasuaji, sambamba na kuimarisha uwezo wa wataalamu wa afya kupitia kubadilishana uzoefu, ujuzi na ushirikiano wa kitaaluma.

"ECSA Health Community kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imefanikiwa kukusanya dola za Marekani 100,000, sawa na takribani shilingi milioni 265, kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania za kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote kupitia ushirikiano wa kikanda" amesema Dkt. Kapologwe

Ameeleza kuwa mpango huo unatarajiwa kuwa endelevu na kupanuliwa katika nchi nyingine wanachama wa ECSA Health Community, ikiwemo Malawi na Kenya, kwa lengo la kuendelea kusogeza huduma za kibingwa na ubingwa bobezi karibu na wananchi pamoja na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma za afya katika ukanda huo.

Aidha, amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo unaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuimarisha mifumo ya afya, kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma bora za upasuaji na matibabu bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.