WANANCHI ZAIDI YA 500 KUNUFAIKA NA HUDUMA ZA KIBINGWA NA UBINGWA BOBEZI
Posted on: July 20th, 2026Na Andrea Kadege, WAF-Arusha
Wananchi zaidi ya 500 wanatarajiwa kunufaika na huduma za kibingwa na Ubingwa bobezi zitakazotolewa kupitia kambi maalumu iliyoanza leo Julai 20 mpaka 30, 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Arusha Mount Meru na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Kusini Mtwara, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
Kauli hiyo imetolewa wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo, na Naibu Katibu Mkuu anayeshughukikia Dawa na Vifaa Tiba Wizara ya Afya, Bw. Emmanuel Tayari, amesema huduma hizo ni za upasuaji wa kibingwa, zikiwa na lengo la kupunguza mzigo kwa wagonjwa waliokuwa wakisubiri huduma hizo na kuwapa fursa ya kupata matibabu bila kusafiri umbali mrefu.
"Serikali imejipanga kuhakikisha utaalamu wa kitabibu unawafikia wananchi walipo badala ya wao kulazimika kufuata huduma hizo mbali, akisisitiza kuwa haki ya kupata huduma bora za afya haipaswi kuamuliwa na umbali wa eneo analoishi mwananchi au uwezo wake wa kifedha" amesema Bw. Tayari
Amesema kuwa kwa muda mrefu baadhi ya wananchi walilazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za kibingwa, huku wengine wakichelewa kupata matibabu au kuuza mali zao ili kugharamia matibabu ambapo kupitia kambi hizo, Serikali inalenga kubadili hali hiyo kwa kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.
Aidha, aliishukuru Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA Health Community) kwa ushirikiano wa kiufundi na wa kimkakati uliofanikisha kufanyika kwa kambi hizo, akibainisha kuwa changamoto za afya zinahitaji ushirikiano wa kikanda unaowezesha kubadilishana wataalamu, maarifa, teknolojia na uzoefu.
Bw. Tayari ametumia jukwa hilo kwa kusema, mafanikio ya kambi hiyo hayatapimwa kwa idadi ya wagonjwa watakaofanyiwa upasuaji pekee, bali pia kwa kiwango cha ujuzi kitakachobaki kwa wataalamu wa ndani ili waendelee kutoa huduma za kibingwa.