Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TAASISI ZA UMMA ZATAKIWA KUHAKIKISHA MIFUMO INASOMANA

Posted on: June 23rd, 2025

Na. WAF, Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amezitaka Taasisi zote za Umma nchini kuhakikisha kuwa mifumo yote wanayoianzisha inasomana ili kubadilishana taarifa.

Waziri Majaliwa ameyasema hayo Juni 23, 2025 wakati akifunga maadhimisho ya kitaifa ya wiki ya utumishi wa umma 2025, jijini Dodoma yaliyoenda na kauli mbiu “ himiza matumizi ya mifumo ya kidijiti ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na kuchagiza uwajibikaji.”

Amesema kusomana na kubadilishana taarifa kwa taasisi za umma kutasaidia utoaji wa huduma kwa haraka na urahisi kwa wananchi na kurahisisha utendaji kazi kwa watumishi.

Aidha, Mhe. Majaliwa amewahimiza watumishi wa umma kuzingatia miiko na maadili ya utumishi wa umma ambayo yanahitaji ukarimu, kuwapokea, kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi ipasavyo.

“Katika kutoa huduma kwa wananchi pia mnatakiwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na miongozo ya idara na kada husika,”amesisitiza Mhe. Majaliwa.

Hata hivyo amewataka viongozi kuandaa uwezeshwaji wa kuelewa mifumo ya kiumma kwa kwa watumishi pamoja na kutenga bajeti ili kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya wiki ya watumishi wa umma ikiambatana na kuweka mikakati ya kutoa huduma na elimu kwa wananchi wanaojitokeza.

katika hatua nyingine Waziri Majaliwa amewataka viongozi, watumishi wa umma na wananchi wote kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka lakini pia kujitokeza kugombea katika uongozi wanaotamani kugombea.