WIZARA, TAASISI ZA KISEKTA KUWEKA JITIHADA ZA PAMOJA KUKABILI DHARURA ZA KIAFYA
Posted on: June 25th, 2025
Na. WAF, Morogoro
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amezihimiza wizara na taasisi za kisekta kuweka jitihada za pamoja ili kukabiliana na dharura za kiafya.
Dkt. Magembe amebainisha hayo Juni 25, 2025 mkoani Morogoro wakati akifungua kikao kazi cha kufanya tathmini ya vihatarishi vya matukio ya dharura kwa afya ya jamii kilichoandaliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO).
"Nimefurahi kuona kikao hiki kimegusa sekta zote, kama vile Maliasili na Utalii, Mipakani, Maji, Kilimo, Usalama Barabarani na Zima Moto, lengo ni sote kuja na kauli moja ya kuweka mikakati ya kujikinga na vihatarishi vya matukio ya dharura ya kiafya kwa sababu sote tunalinda taifa moja na lazima tujipange kama nchi kukabiliana na majanga ieleweka kuyakabili majanga hauwezi kufanya peke yako, tushirikiane, wizara na taasisi za kisekta tuweke jitihada za pamoja,” amesema Dkt. Magembe
Aidha, Dkt. Magembe amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya afya kwa jamii kujikinga na majanga ikiwemo magonjwa ya mlipuko sambamba na kuwa na desturi ya kufanya tathmini mara kwa mara kwenye utekelezaji wa mikakati ya kupambana na kuzuia athari za majanga na magonjwa kutoingia nchini.
"Suala la elimu ya afya ni muhimu sana mfano, wananchi kuacha kuwapa mifugo dawa za binadamu, lakini kuzingatia matumizi sahihi ya dawa ili yasilete tatizo la usugu wa dawa, namna gani jamii inaweza kujikinga na kipindupindu na kuacha mila na desturi potofu,” amesema Dkt. Magembe
Kwa Upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Dharura kutoka Wizara ya Afya Dkt. Erasto Sylvanus amesema kikao hicho kina mchango mkubwa kwenye suala la dharura ya afya ambapo wanajadili majanga ya asili na magonjwa ya mlipuko na namna ya kukabiliana nayo ili kupunguza au kuzuia majanga.
Naye, Mtaalam wa Udhibibiti wa Dharura na na Majanga ya Afya kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Faraja Msemwa amesema suala la udhibiti wa majanga sio la Wizara ya Afya pekee hivyo WHO inahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na majanga ya dharura za kiafya.