SERIKALI KUBORESHA HUDUMA ZA MAABARA ILI KUIMARISHA UFUATILIAJI MAGONJWA
Posted on: June 23rd, 2025
Na WAF - MOROGORO
Serikali imedhamiria kuendelea kuimarisha uwezo na huduma za Maabara nchini ili ufutiliaji wa magonjwa mbalimbali nchini sambamba na ya mlipuko iweze kusaidia kuimarisha huduma na kulinda Afya za wanaanchi.
Hayo yamebainishwa leo Juni 23, 2025 mkoani Morogoro na Mkuu wa Huduma za Maabara Wizara ya Afya Bw. Reuben Makala wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya kuandaa zana ya ufuatiliaji wa magonjwa yanayoathiri binadamu sambamba na yale ya mlipuko.
Mafunzo hayo ambayo yamejumuisha wataalam kutoka Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais - TAMISEMI yamepangwa kufanyika kwa siku tano (5) kuanzia Juni 23-27, 2025 ambapo Bw. Makala amesisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia muda ili kufanikisha malengo waliyojiwekea.
Bw. Makala amewataka wanufaika wa mafunzo hayo kuhakikisha wanayafikisha kwa watumishi wengine kwenye maeneo yao.
“Kikubwa baada ya mafunzo haya tuone matokeo, tutakapokumbana na changamoto yoyote ya milipuko Tanzania tuwe mbele tukiongozwa na wataalam ambao wana uelewa na uzoefu wa kukabiliana na haya magonjwa lakini pia hata kuibua magonjwa mbalimbali yaliyoko kwenye jamii na vituo vyetu hasa maabara,” amesema Bw. Makala.
Kwa upande wake Mratibu wa mafunzo hayo Bw. Joackim Chacha amesema wameandaa mafunzo hayo na kikao kazi hicho cha kuandaa Nyenzo za kufundishia watumishi wa afya ili kuwaimarisha katika ukusanyaji, uandaaji, uhifadhi na utoaji taarifa za uchunguzi wa magonjwa kwa kuzingatia miongozo ya kitaifa na kimataifa.
“Sasa hivi tupo kwenye hatua za kuimatisha huduma za maabara nchini ili kuhakikisha maabara inafanya kazi zake vizuri zaidi katika kukabiliana na magonjwa hapa nchini, maabara ni sehemu ambayo inaweza ikatupatia viashiria vya uwepo wa dharura yoyote hapa nchini, na tunafahamu mchango wa wataalam wa maabara katika kutoa huduma kwa wananchi,” amesema Bw. Chacha.
Mafunzo hayo ni muendelezo na juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za maabara kwa kuwajengea uwezo watumishi wa Afya, ili kuongeza ufanisi na kufikia viwango vya ubora vinavyotakiwa hasa wakati wa dharura za milipuko.