Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

VYOMBO VYA HABARI NCHINI VYATAKIWA KUZINGATIA SHERIA ZA URUSHAJI MATANGAZO YA TIBA ASILI, MBADALA

Posted on: June 29th, 2025

Na. WAF, Morogoro

Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini limevitahadharisha vyombo vya habari vinavyoendelea kurusha vipindi na matangazo yanayohusu tiba asili bila kibali, licha ya kuwepo kwa maelekezo ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) yanayovitaka kuzingatia taratibu jambo ambalo ni ukiukaji wa sheria unaoweza kuhatarisha maisha ya wananchi.

Tahadhari hiyo imetolewa leo Juni 28, 2025 mkoani Morogoro na Mwenyekiti wa Baraza hilo Prof. Joseph Otieno, wakati akifungua semina ya siku moja kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali.

Amesema baadhi ya matangazo yanayorushwa yamejaa upotoshaji kuhusu uwezo wa waganga kutibu magonjwa sugu, jambo ambalo halijathibitishwa kitaalam.

“Tangazo lolote linalohusiana na tiba asili ni lazima lipitie kwa Msajili wa Baraza kabla ya kurushwa,” amesema Prof. Otieno.

Naye, Msajili wa Baraza hilo, Bi. Lucy Mzirai, ameisistiza jamii kupuuza matangazo ya mitandaoni na yale ya mitaani yasiyo na uthibitisho, na badala yake kufuata huduma katika vituo vya afya na Hospitali zinazotambulika kisheria.

“Hadi sasa, zaidi ya dawa 127 za asili zimesajiliwa, katika mwaka wa fedha 2025/26 huduma hiyo itatolewa kwenye hospitali 14 zikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Morogoro, Temeke, Dodoma na Mount Meru,” amesema Bi. Lucy

Ameongeza kuwa zaidi ya tani 30 za dawa za tiba asili huuzwa nje ya nchi kila mwaka, na kuingizia Taifa wastani wa dola 200,000 sawa na Shilingi Milioni 520 kwa mwaka.