Wizara Ya Afya

TAKWIMU SAHIHI NI MSINGI WA UTEKELEZAJI BORA WA AFUA ZA NTD - DKT. MWANSASU

Posted on: March 6th, 2026

Na WAF, Morogoro

Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTD) kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Clara Mwansasu, amesema utoaji wa takwimu sahihi na kwa wakati ni msingi muhimu wa utekelezaji bora wa afua za Magonjwa hayo nchini.

Dkt. Mwansasu amesema hayo Machi 04, 2026 mkoani Morogoro katika kikao cha kuhuisha taarifa za Kadi ya Alama (Score Card) ya NTD kilichoratibiwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na OWM -TAMISEMI na Muungano wa Viongozi wa Kupambana Malaria Afrika, African Leaders Malaria Alliance (ALMA),

Dkt. Mwansasu amesema kuwa uboreshaji wa takwimu ni hatua muhimu katika kuongeza uwajibikaji na ufanisi wa utekelezaji wa afua za Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele nchini.

"Kadi ya Alama ni nyenzo muhimu inayosaidia kuonesha hali halisi ya utekelezaji wa mipango katika mikoa, kubaini mafanikio pamoja na changamoto zilizopo, na kuweka mikakati ya maboresho kwa wakati," amesema Dkt. Mwansasu

Aidha, Dkt. Mwansasu amesema kadi ya alama itatuonesha tulipo na namna gani ya kuongeza uwajibikaji katika kuboresha huduma.

Kwa upande wake, Afisa Mpango anayeratibu Ufuatiliaji, Tathmini na Tafiti kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele, Dkt. Stephen Mbwambo, amesema kikao hicho kimewapa fursa waratibu wa NTD pamoja na waratibu wa takwimu za Afya ngazi ya mkoa (HMISFP) kujadili juu ya upatikanaji, uchakataji na uhakiki ubora wa takwimu ili kuhakikisha zinakuwa sahihi, kamili na zenye kuaminika katika kufanya maamuzi sahihi.

Nae, Mratibu wa NTD Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI Dkt. Irene Haule amesema kuhuisha takwimu za Kadi ya alama ni muhimu katika kuimarisha utekelezaji wa kukabiliana na magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.

Kikao hicho kimewakutanisha Waratibu wa Mikoa wa NTD na Maafisa Takwimu ngazi ya Mkoa kwa lengo la kujengewa uwezo wa matumizi ya takwimu katika kupanga, kufuatilia na kutathmini afua mbalimbali za magonjwa hayo.