NCHI 14 ZANUFAIKA NA MAFUNZO YA MATENGENEZO KINGA KUTOKA MAABARA YA TAIFA
Posted on: March 10th, 2026Na Atley Kuni- WAF, Dar es Salaam
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya imeendelea na jitihada za kuwajengea uwezo wataalam wa maabara kutoka nchi 14 wanachama wa umoja wa Afrika ikiwa na malengo ya kuhakikisha wanakuwa na malengo yanayofanana katika utoaji wa huduma za maabara.
Mapema juma hili, Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa Bw. Ambele Mwafulango, akifungua mafunzo ya siku kumi jiji Dar es Salaam, amewataka wataalam hao kuzingatia wanatumia siku hizo kumi watakazowepo kwenye mafunzo wanatoka wakiwa wameiva.
“Ni imani yangu baada ya mafunzo haya, kila mmoja wetu atakuwa na uelewa mpana juu ya Uteuzi, Ufungaji, Matengenezo na Udhibiti ubora wa Makabati ya usalama (Biological safety cabinets), amesema Bw. Mwafulango.
Bwana Mwafulango amesema, mbali na kupata maarifa na ujuzi, vilevile italisaidia bara la Afrika kuwa na wataalam wake wenyewe wanaojitosheleza na kuachana na utegemezi katika suala zima la kuhudumia maabara za nchi wanachama.
Mafunzo hayo ya siku kumi kwa wataalam wa Maabara na Vifaa tiba yameandaliwa na Wizara ya Afya kupitia kituo cha umahiri cha kikanda katika eneo la ulinzi na usalama wa vimelea hatarishi vya kibailojia kwa udhamini African Centre for Disease Control and Prevention.