Wizara Ya Afya

HOSPITALI ZIWEKE MIFUMO YA MREJESHO KUTOKA KWA WAGONJWA

Posted on: March 6th, 2026

Na Shaban Juma, WAF-Mbeya

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amezielekeza hospitali nchini kuanzisha mifumo ya kupata mrejesho wa matibabu kutoka kwa wagonjwa ili kufahamu namna huduma za afya zinavyotolewa na kubaini maeneo yanayohitaji kuboreshwa.

Dkt. Samizi ametoa maelekezo hayo leo Machi 05, 2026 wakati wa ziara yake katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, ambapo amesema uwepo wa mifumo ya maoni kutoka kwa wagonjwa utasaidia kuongeza uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Aidha, amesema ni muhimu hospitali kuwa na vitengo madhubuti vya huduma kwa mteja ili kupokea maoni, malalamiko na mapendekezo ya wagonjwa na kuyafanyia kazi kwa wakati ili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ubora unaostahili.

Katika hatua nyingine, Dkt. Samizi amewataka wakuu wa idara katika hospitali kusikiliza na kushughulikia changamoto za watumishi wao ili kuweka mazingira mazuri ya kazi yatakayowawezesha kufanya kazi kwa weledi na ufanisi.

Pia amesisitiza umuhimu wa mifumo ya hospitali kusomana ili kudhibiti mapato, akieleza kuwa kuna baadhi ya watu wanaojiandikisha kupata huduma lakini si wao wanaopatiwa matibabu, hali inayoweza kusababisha upotevu wa mapato na hasara kwa taasisi.

Dkt. Samizi amesema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwekeza katika kuboresha huduma za afya ili wananchi wapate huduma bora na zenye kuleta tabasamu.

Sambamba na hilo, ametoa wito kwa wataalamu wa afya kuendelea kutoa elimu ya afya kwa jamii kuhusu huduma zinazotolewa hospitalini kupitia njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma hizo.