Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WANANCHI SONGEA DC WAHIMIZWA KUZINGATIA CHANJO DHIDI YA MAGONJWA

Posted on: June 28th, 2025

Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea   wametakiwa kuzingatia chanjo  zinazotolewa kwa watoto chini ya miaka mitano na mabinti wenye umri wa miaka tisa ili kujikinga na magonjwa yanayoweza kuzuilika.


Rai hiyo imetolewa leo Juni 27, 2025 na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, Dkt. Otilia Gowelle wakati akifungua semina ya kuelimisha na kuhamasisha wananchi wa wilayani humo kuhusu umuhimu wa chanjo mbalimbali zinazotolewa ili kujikinga na magonjwa yanayoweza kuzuilika.


"Chanjo ni mkakati muafaka katika kutokomeza magonjwa na kupinguza vifo vya  watoto hivyo kupunguza gharama kubwa ambazo familia  na taifa kwa ujumla ingetumia katika kutibu magonjwa ambayo yanazuilika kwa chanjo," amefafanua Dkt. Gowelle.


Dkt. Gowelle amesema  Wizara ya Afya kupitia Mapango wa Taifa wa Chanjo inaratibu utoaji wa chanjo za kukinga dhidi ya magonjwa ya kifua kikuu, polio, dondakoo, kifaduro, surua, rubella, pepopunda,, homa ya ini, homa ya uti wa mgongo, kichomi, kuhara kukali, saratani ya mlango wa kizazi na mafua makali.


Aidha ameeleza kuwa imethibitishwa kuwa chanjo huzuia takribani vifo milioni 2 hadi 3 kila mwaka kutokana na maradhi yanayozuilika kwa chanjo duniani.


Ameongeza kuwa nchini Tanzania hali ya chanjo imefikia asilimia 96, hivyo kuwa katika hali nzuri, hata hivyo bado kuna umuhimu wa kuendela kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kuhusu masuala ya chanjo ili kufikia asilimia 100.


Amebainisha kuwa mafanikio hayo makubwa yametokana na juhudi za  Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama  kwa kuweka kipaumbele namba moja masuala ya afya hususan chanjo za watoto zinazowakinga dhidi ya magonjwa yanayozuilika.


"Serikali inatoa chanjo hizi bila malipo katika vituo vinavyotoa huduma za chanjo vya Serikali, vya binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali, huduma za mkoba na tembezi katika jamii," amefafanua Dkt. Gowelle.


Hata hivyo, amewataka wananchi kuhamasisha zaidi  kuhusu chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa mabinti wenye  umri wa miaka tisa (9) Hadi Miaka 14 kwani katika baadhi ya maeneo mwitikio umekuwa ni mdogo.


Awali akizungumza ofisini kwake Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Bi. Mary Gasper Makondo amesema mkoa umekuwa ukifuatilia kwa ukaribu masuala ya chanjo kwa kutoa elimu na kuhamasisha ikiwa ni pamoja na shuleni lengo likiwa ni kuwa na uwelewa wa pamoja kuhusu chanjo.