Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI YAENDELEA KUPIGA HATUA KUPUNGUZA MALARIA NCHINI.

Posted on: June 28th, 2025

Na. WAF, Dodoma.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau imepiga hatua kubwa katika kupunguza ugonjwa wa Malaria kwa kutekeleza afua mbalimbali za kupambana na ugonjwa huo, hali iliyowezesha kuokoa vifo vya akina mama na watoto waliokuwa wanapoteza maisha kutokana na malaria.

Mhe. Balozi Kombo ameyasema hayo Juni 28, 2025 jijini Dodoma wakati akitia saini ya mkataba wa uwenyeji kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Taasisi ya Umoja wa Wakuu wa Nchi za Afrika (ALMA) dhidi ya Malaria, jijini Dodoma.

Amesema Serikali ya Tanzania inaendelea na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria katika mazalia ya mbu waambukizao Malaria, kinga na tiba lengo likiwa ni kutokomeza kabisa ugonjwa huo.

“Serikali kupitia wizara ya afya imefanya kazi kubwa sana kwa kupambana kupunguza malaria, sasa hivi ukiuliza mtu mmoja mmoja mara ya mwisho kuugua malaria ni lini utagundua ni zaidi ya miaka hajaugua, hata mimi mwenyewe nina zaidi ya miaka mitano sijaugua malaria, hivyo inatoa takwimu kwa kila mmoja kuwa malaria imepungua kwa kiasi kikubwa sana,” amesema Mhe. Balozi Kombo.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe akimwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema, uwepo wa makao makuu ya taasisi ya ALMA nchini kutasaidia kunufaika katika mipango inayopangwa kwa ajilii ya kusaidia nchi za Afrika dhidi ya malaria lakini pia wataalam wa Tanzania kuingia kwenye sekretarieti ya ALMA kujadili mambo mbalimbali yanayohusu malaria na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na ALMA tutaendelea kuyapa kipaumbele na hatimae kutokomeza malaria ifikapo 2030.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Taasisi ya ALMA,
Bi. Joy Phumaphi amesema makubaliano ya nchi mwenyeji yaliyosainiwa leo siyo tu taratibu za kisheria bali ni ishara ya ukuaji endelevu wa ALMA na uongozi wa Tanzania katika diplomasia ya afya ya kikanda na ya bara zima