Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WANANCHI ZAIDI YA 700 KUREJESHEWA UONI RUNGWE

Posted on: June 25th, 2025

N, WAF – Mbeya


Wananchi zaidi ya 700 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho kupitia kambi maalum ya matibabu ya macho.


Hayo yameelezwa leo, Juni 25, 2025 na Mganga Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Dkt. Elizabeth Nyema wakati akifungua kambi ya matibabu ya mtoto wa jicho inayoendelea wilaya ya Rungwe mkoa Mbeya. 


Katika Kambi hiyo iliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali, Shirika la Helen Keller, na Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mbeya, Dkt. Nyema amesema lengo ni kuondoa ulemavu wa kutokuona na kuwarejeshea wananchi uwezo wa kuona.



“Ili kuwafikia wahitaji kwa ufanisi, tumetumia mbinu ya kuwafuatilia kaya kwa kaya kwa msaada wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii. Njia hii imewezesha kuwabaini wananchi wengi waliokuwa wakihitaji matibabu lakini hawakuwa na taarifa sahihi. Ushirikiano wa karibu na jamii umeongeza ufanisi wa zoezi hili,” amesema Dkt. Nyema. 


Aidha, Watumishi zaidi ya 15 wamejengewa uwezo na wanaporudi kwenye maeneo yao waendelee kutoa huduma.


“Hii inaonesha ukubwa wa tatizo na umuhimu wa kuendelea na huduma hizi za kambi, wananachi  hawa sasa wana matumaini ya kurejesha uwezo wao wa kuona,” amesema Dkt. Nyema.


Kwa upande wake, Afisa kutoka mpango wa Taifa wa Macho, Wizara ya afya , Dkt. Eunice Headcraph  amesema kipaumbele kimojawapo cha Wizara ni kuendelea kuwafikishia huduma za Afya ya macho karibu zaidi na wananchi hivyo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi na kutumia fursa ya uwepo wa kambi hizo katika maeneo yao kujua afya zao na kupatiwa matibabu. 


Dkt. Eunice ameushukuru uongozi wa wilaya ya Rungwe, mkoa wa Mbeya na Shirika la Helen Keller International kwa ushirikiano wao kwenye kampeni hiyo na kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuwafikishia wananchi huduma ya matibabu ya upasuaji wa mtoto wa jicho bila malipo.