Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HAKIKISHENI MNAWAFAHAMU VIZURI MNAOWAONGOZA KUEPUSHA MIGOGORO

Posted on: December 14th, 2024

Na WAF , Mbeya

Wakuu waIdara Sekta ya Afya wametakiwa kuwafahamu kwa undani watu wanaowaongoza ili kujiepusha na migongano mbalimbali inayoweza kuathiri utendaji kazi katika maeneo yao ya kazi.

Hayo yamesemwa Desemba 13, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili cha kufanya tathmini na kubadilishana uzoefu wa utekelezaji wa njia bora za kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi, mama na mtoto kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi inayohusisha mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa.

"Hakikisheni mnawafahamu watu mnaowaongoza vizuri na usiruhusu kupambana na mtu, jitahidi upate kibali kwao kitakachokuwezesha wakuunge mkono,” amesema Dkt. Mbwanji.

Aidha, Dkt. Mbwanji amewataka watumishi kutotenganisha furaha na kazi kwakuwa ni muhimu kufanya hivyo hasa kwa kuwapa nafasi wanaowaongoza kwani ni njia bora ya kupunguza msongo wa mawazo na kuongezeka kwa hamasa katika utekelezaji wa majukumu yao wawapo maeneo ya kazi.

Akiongea kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Lighton Alex amewataka washiriki wa kikoa kazi hicho kuhakikisha mambo yote yaliyojadiliwa yanatekelezwa kwakuwa kwasasa Serikali haidaiwi kitu zaidi ya huduma bora kutoka kwa watumishi hao.

Kwa upande wake Afisa Mradi kutoka Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Dkt. Joachim Masunga amewaasa watumishi sekta ya Afya kuwa na ushirikiano katika maeneo mbalimbali hasa eneo la takwimu ili kupata takwimu sahihi za mkoa zitakazorahisisha utekelezaji wa majukumu yao.

"Nendeni mkashirikiane kwenye maeneo yote hasa kwenye eneo la takwimu kwakuwa takwimu za mkoa ni za kwenu wote,” amesema Dkt. Joachim Masunga

Naye Mratibu wa Afya yab Uzazi na Mtoto Kandanl ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi, Bi. Magdalena Swebe, ameshukuru kwa niaba ya viongozi mbalimbali waliohudhuria kikao hicho na kuahidi kuwa yale yote yaliyojadiliwa yatakwenda kutekelezwa ili kuwa mfano kwa watumishi wa chini wanaowaongoza.