Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI YAENDELEA KUDHIBITI USAMBAAJI VIMELEA VYA MALARIA KWA WATOTO WA SHULE.

Posted on: May 23rd, 2025

Na WAF - DODOMA


Serikali imeendelea kudhibiti vimelea vya malaria katika maeneo ya shule za msingi kwa wanafunzi wa darasa la kwanza mpaka la saba, ambao baadhi yao bila kujua wamekuwa  wakitembea  na vimelea vya malaria na kuwaambikiza wengine au kusambaza katika maeneo ya shule au kurejesha maambukizi majumbani.


Hayo yamebainishwa na Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wa kudhibiti Malaria Dkt. Abdallah Lusasi wakati wa kikao cha mrejesho cha wadau wa Malaria Nchini kilichofanyika Mei 23, 2025 Mkoani Dodoma.


 Dkt. Lusasi  amesema katika kutatua hilo serikali imetoa tiba kinga kwa watoto hao wa shule katika maeneo mbalimbali nchini.


“Tuna tiba kinga kwa watoto wa shule za msingi na tunawapa katika vipindi maalum vya maambukizi wa ugonjwa wa malaria, sasa hivi tunaendelea Nyang’wale na Kibondo, na maeneo yenye maambukizi ya juu,” amesema Dkt. Lusasi


Pia amesema Serikali imedhamiria kupunguza hali ya maambukizi ya malaria kufikia asilimia 3. 5 hadi kufikia mwisho wa mwaka 2025 kwa nchi nzima na kuitokomeza malaria kabisa ifikapo 2030.



“Tuendelee kushirikiana kwa pamoja na wananchi kule chini, asasi za kijamii na kiraia kwakuwa  mko karibu na jamii na nyinyi ndio nyenzo wezeshi za kufanikisha hili  la kupambana na Malaria na kuitokomeza ifikapo 2030,”  amesema Dkt. Lusasi.


Ameongeza kuwa iwapo ushirikiano baina ya Serikali, wadau na jamii utaendelea kuzingatia nguzo za udhibiti wa malaria kwa kila kundi kutimiza wajibu wake na jukumu lake la msingi lengo hilo litafikiwa kwa ushirikiano baina ya Serikali, wananchi na asasi za kiraia.



Amegusia pia suala la umuhimu wa matumizi ya takwimu zinvyosaidia kutoa mwelekeo wa mapambano, uelimishaji umma katika kutokomeza malaria sambamba na upatikanaji wa dawa na bidhaa tiba zote za Malaria.