USHIRIKIANO WA WADAU UMEPUNGUZA VIFO VYA WAKINA MAMA, WATOTO TANZANIA
Posted on: May 22nd, 2025
Na WAF - Geneva, Uswisi
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ameelezea mafanikio ya Tanzania yanayopatikana yanatokana na ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na wadau ambayo ni pamoja na kupungua kwa vifo vya kina mama wajawazito pamoja na watoto wachanga.
Waziri Mhagama ameeleza hayo wakati akifanya mazungumzo na Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya ya Laerdal Global Health, Bw. Tore Laerdal, ambao ni wadau wakubwa katika sekta ya afya nchini Tanzania.
"Serikali ya Tanzania imejidhatiti katika kuboresha afya na ustawi wa wanawake na wasichana pamoja na watoto ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili kwa kulenga maeneo ya kuimarisha mifumo ya afya kama ilivyoainishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO)," amesema Waziri Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagama amesema Serikali ya Tanzania imeanzisha mikakati mbalimbali ya kuboresha afya za wanawake na wasichana, ikiwemo kuboresha mfumo wa fedha za afya, kuanza utekelezaji wa huduma ya afya kwa wote.
"Lakini pia tumeanza uboreshaji wa mfumo wa rufaa za dharura kama vile mradi wa m-mama, kufanya tathmini na ufuatiliaji wa vifo vya kina mama na watoto, kuboresha ubora wa huduma kwa wanawake, wasichana na watoto wachanga, kuimarisha ujuzi wa wahudumu wa afya kupitia mafunzo na mazoezi ya vitendo," amesema Waziri Mhagama.
Katika kikao hicho wamekubaliana kuendeleza ushiriikiano baina ya Taasisi hiyo na Serikali ya Tanzania ili kuboresha zaidi katika maeneo hayo.