Wizara Ya Afya

SERIKALI YAIMARISHA MIKAKATI YA KINGA YA MAGONJWA KWA TAFITI ZA KISAYANSI

Posted on: March 15th, 2026

Na Mvuda Jaffer,WAF-Morogoro

Umuhimu wa ushirikiano wa Taasis za Utafiti na Wizara ya Afya katika ufuatiliaji na Udhibiti wa Magonjwa umeelezwa kuwa mkakati wa makusudi unaochikuliwa na Wizara ya Afya kwa muda wote. Lengo ni kuwa na njia madhubuti inayoboresha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa na kuharakisha utambuzi na uchukuaji hatua kwa wakati na haraka kupata matokea ya tafiti zinazofanywa na taasisi za utafiti.

Hayo yameelezwa leo Machi 14,2026 mkoani Morogoro na Kaimu Mkurugenzi wa huduma za Kinga, Dkt.Amour Seleman wakati wa kikao cha kukamilisha taarifa ya kitaalamu baada ya zoezi la kutambua njia na mienendo ya watu wanaoingia na kutoka nchini kupitia mipaka rasmi na isiyo rasmi ya mikoa ya Kigoma na Rukwa na kuandaa machapisho ya matokeo ya tafiti zilizofanyika.

“Lengo la tafiti mara nyingi ni kutafuta mbinu mbadala zinazoongeza ufanisi wa mifumo. Hivyo inakua ni vema na faida kubwa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za utafiti na Wizara katika kupata na kutumia mbinu bora na zenye matokeo katika kufuatilia na kudhibiti magonjwa katika maeneo yote ikiwamo mipakani.”amesema Dkt.Seleman

Naye Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Ardhi Dkt. Jonas Gervas amesema taasisi hizi zinaweza kushirikiana katika kuandaa machapisho na nyaraka za kitaalamu zinazotoa taarifa na ushauri kuhusu viashiria vinavyoweza kuchochea maambukizi ya magonjwa mipakani, kuandaa miongozo na mipango mikakati ya kudhibiti magonjwa, pamoja na kuandaa maandiko ya miradi na mapendekezo ya ufadhili yatakayosaidia kupata rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa programu za kudhibiti maambukizi.

“Ushirikiano huu unaimarisha ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kudhibiti magonjwa, kuandaa kwa pamoja taarifa za utekelezaji wa mipango ya kila mwaka au ya programu maalum, pamoja na kuweka malengo ya pamoja ya kudhibiti magonjwa mipakani. “amesema Dkt.Gervas

Ushirikiano huu husaidia kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa taarifa, upangaji wa mikakati na utekelezaji wa hatua za afya ya jamii katika maeneo ya mipaka.