WATALAAM WA AFYA MAMA NA MTOTO WAJENGEWA UWEZO, KUONGEZA UFANISI MATUMIZI YA VIFAA TIBA
Posted on: March 13th, 2026Na Emmanuel Malegi, WAF- Morogoro
Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kutekeleza jitihada za kuboresha afya ya uzazi, mama na mtoto ili kufikia malengo ya Kitaifa na Kimataifa ikiwemo mpango wa tano wa Maendeleo ya sekta ya Afya (HSSP-V) na malengo ya Maendeleo endelevu (SDG's) kwa kuwajengea uwezo Wataalam wa afya ya mama na mtoto kwenye matumizi ya vifaa tiba.
Akizungumza Machi 12, 2026, mkoani Morogoro Mratibu wa mafunzo Dkt. Angela Leonard amesisitiza matumizi sahihi ya vifaa tiba vya afya ya uzazi vya huduma za afya ya mama na mtoto ili viweze kudumu vikiwa na ufanisi ili kuongeza usalama wa wagonjwa pamoja uwajibikaji ikiwa ni kipaumbele cha Serikali kufikisha huduma hizo karibu na wananchi.
Dkt. Angela amesema kuimarika kwa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto kunaenda sambamba na utekelezaji wa afua zake ikiwemo wataalam wa afya kujengewa uwezo ili waweze kutoa huduma bora kwa wazazi na Watoto wanaofika vituo vya afya ili kupata huduma.
“Katika jitihada hizo, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wa huduma za afya imeweka jitihada kuhakikisha vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto vinapatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya”, amesema Dkt. Angela.
Ameongeza kuwa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na “The Hatch Technology & ANUDHA” imeandaa mafunzo hayo ya matumizi ya vifaa tiba vya afya ya mama na mtoto kwa watoa huduma.
Mafunzo hayo yamehusisha Wataalam wa afya kutoka Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Wilaya na vituo vya afya katika Mikoa 23 nchini.