HALMASHAURI ZOTE 184 NCHINI KUANZA MCHAKA MCHAKA MASHINDANO YA USAFI WA MAZINGIRA 2026
Posted on: March 15th, 2026Na Happyness Hans, WAF – Dodoma
Wizara ya Afya inaendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za Afya na Usafi wa Mazingira nchini kwa lengo la kulinda jamii dhidi ya magonjwa yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira. Jitihada hizi zinalenga kuhamasisha jamii kqa pamoja na wadau kushiriki kikamilifu katika kuboresha hali ya usafi wa mazingira nchini.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Usafi wa Mazingira, Bw. Anyitike Mwakitalima, wakati akitoa mafunzo rejea kwa wahakiki wa Mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira Tanzania Bara kwa mwaka 2026, yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara ya Afya jijini Dodoma.
Mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira kwa mwaka wa fedha 2025/26 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Mtu ni Afya, Dumisha Usafi wa Masoko.”
Ameeleza kuwa mashindano hayo hufanyika kwa kushirikisha Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na taasisi mbalimbali katika mikoa yote ya Tanzania Bara, ambapo halmashauri zitakazofanya vizuri hutambuliwa na kupewa zawadi kama motisha ya kuendelea kuboresha usafi wa mazingira.
“Kwa mwaka huu, Wizara imepanga kufanya uhakiki wa mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza ilihusisha Majiji, Manispaa na Miji, huku awamu ya pili ikitarajiwa kufanyika katika halmashauri zote nchini kuanzia Machi 8 hadi Machi 30, 2026, ikihusisha mikoa yote ya Tanzania Bara,” amesema Bw. Mwakitalima.
Aidha, amewasisitiza wahakiki wote kuzingatia uadilifu wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, akiwataka kuepuka vitendo vya rushwa, upendeleo au vitisho kwa mtu yeyote ili kuhakikisha tathmini inafanyika kwa haki na kutoa matokeo sahihi.