Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI, WADAU WAJIPANGA KUDHIBITI MILIPUKO YA MAGONJWA KABLA HAYAJATOKEA

Posted on: May 22nd, 2025

Na WAF Morogoro


Serikali na wadau wa sekta ya afya inaendelea kufanya jitihada za kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa ya milipuko kwenye ngazi zote, kwa lengo la kuzuia na kudhibiti milipuko ya magonjwa kwa wakati.


Hayo yamebainishwa   Mei 21, 2025 mkoani Morogoro na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Dharura na Maafa, Dkt. Erasto Sylvanus wakati wa kikao kazi cha  kutathmini mipango na mikakati iliotumika kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Marburg nchini katika wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera na kuweka mipango na mikakati ya baadaye kudhibiti ugonjwa huo na mengine yasitokee.


Dkt. Sylvanus amesema jitihada zaidi zinafanyika  kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa ili kusaidia kuzuia milipuko ya magonjwa na si kusubiri itokee ili kudhibiti.


“Kupitia kikao kazi hiki, tutajadili kwa kina na kutoka na mpango kazi wenye mapendekezo ya namna ya kukabiliana na milipuko ya magonjwa pindi itakapotokea, Lengo ni kuendeleza yale tuliyofanya vizuri ili tuyadumishe na kuyaimarisha, huku tukihakikisha changamoto zilizojitokeza awali hazijirudii, ili kuongeza ufanisi katika udhibiti wa magonjwa,” amesema Dkt. Sylvanus.


Dkt. Sylvanus ameongeza kuwa, Serikali ilifanya juhudi kubwa kudhibiti virusi vya Marburg kutosambaa nje ya mkoa wa Kagera ndani ya muda mfupi ukilinganisha na nchi jirani zilizokumbwa na virusi hivyo.


Naye Mratibu Udhibiti wa Athari za Majanga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Saumu Nungu amesema nguzo kubwa ya kudhibiti ugonjwa hasa magonjwa ya mlipuko ni ushirikishwaji wa utoaji wa taarifa mapema pale tu zinapoonekana dalili za ugonjwa, hivyo suala la kuwashirikisha wananchi wakati wote litaendelea kuimarishwa. 


"Nitoe rai kwa wananchi wote kuendelea kushirikiana na Serikali katika utoaji wa taarifa  mapema kufuatia hali ya afya katika maeneo yao wanayoishi na kufuata maelekezo na ushauri wanayopewa na wataalam muda wote ili kushiriki na kuimarisha mikakati ya kudhibiti dharura zinapotokea," amesema Dkt. Nungu.


Kwa upande wake Mtaalamu wa Kukabiliana Dharura na Majanga ya Afya kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Faraja Msemwa amesema  Shirika hilo linaendelea kufanya kazi kwa karibu  na Serikali kupitia Wizara ya Afya ili kukabiliana na dharura pamoja na magonjwa ya mlipuko pindi yatakapotokea. 


Aidha, amesema WHO inaendelea kuwaratibu wadau wa sekta ya Afya katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kukabiliana na dharura na majanga ya kiafya