WADAU WATAKIWA KUZINGATIA TAKWIMU SAHIHI KWENYE MAPAMBANO DHIDI YA SARATANI
Posted on: May 22nd, 2025
Na WAF, Dodoma
Kamati ya Ushauri ya Usajili wa Saratani (ACCR) imetoa wito kwa wadau mbalimbali kuwa na mapango madhubuti wa kuwa na takwimu sahihi ili kusaidia Serikali kuweka sera na mikakati sahihi ya kupambana na saratani nchini.
Wito huo umetolewa leo Mei 22, 2025 Jijini Dodoma na mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo ambaye pia ni Meneja Mpango wa Magonjwa yasiyo ya kuambukiza kutoka Wizara ya Afya, Bi. Edith Bakari wakati wa kuhitimisha kikao cha pili baada ya kamati hiyo kuzinduliwa jana jijini hapa.
Bi Edith amesema kamati hiyo itadumu kwa miaka mitatu na itakuwa ikitoa ushauri kwenye masuala ya saratani.
Amesema kamati ina lengo la kukusanya takwimu sahihi za ugonjwa wa saratani ambazo zitasaidia Taifa kupambana na ugonjwa huo kwa ufasaha .
“Kamati zetu hizi tulivyozitengeneza hii itakuwa ni kamati kuu na katika kila kamati kuu kutakuwa na kituo ambacho kitakuwa kinafanya usajili na wa kamati ndogo ambayo itaunganisha vituo vyote vinavyotoa huduma pamoja na wadau bila kusahau wagonjwa ,” ameeleza Bi. Edith.
Amesema kamati kuu pia imejumuisha wagonjwa ili waweze kusikia sauti ya kila mdau na kuwasaidia kuweka mipango sawa ambapo kamati ya vituo itakuwa ikiripoti kwa kamati kuu ili kuchukua takwimu kwa kamati ya kitaifa.
Kwa upande wake mjumbe Dkt. Julius Aloyce kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC, amesema ugonjwa wa saratani unakuwa kwa kasi katika jamii, hivyo lazima kuwe na takwimu sahihi za kuisaidia Serikali kuweka mipago madhubuti ya kupambana na saratani.
“Ni wakati sahihi wa kuona ni namna gani tunaweza kuongeza ufanisi katika magonjwa ya saratani na jinsi ya kuboresha katika jamii ya watanzania,” amesema Mtaalam huyo.
Hata hivyo ametoa wito kwa Watanzania kuwa na utayari wa kujifunza na kupambana na saratani kwa kuhakikisha zinapatikana takwimu sahihi na kwa wakati.
“Kuna sintofahamu mtu anapojulikana ana saratani hii inachagizwa kwa kutokuwa na uelewa kuwa ni janga kubwa hivyo kila mmoja yupo hatarini, hivyo ni jukumu letu kujifunza jinsi ya kuepuka na saratani pamoja na kufanya uchunguzi na hatua zipi za kufuata kwa usahihi,” amesema Dkt. Aloyce.